Baada ya Arusha, Chadema kujifungia Mtwara

Muktasari:

Maandamano ya Arusha yalifuatia yale yaliyofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya


Dar/Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuja na Azimio la Mtwara, ikiwa ni hatua baada ya kumalizika kwa maandamano yaliyofanyika katika majiji manne nchini.

Kwa mujibu wa  Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, msingi wa azimio hilo ni kutoa jawabu la nini kitafuata chenye sura ya mapambano baada ya kumalizika kwa maandamano katika majiji hayo.

Kauli hiyo ya Mbowe inakuja baada ya kuhitimishwa kwa maandamano jana katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha yaliyohusisha matembezi ya jumla ya kilomita 169.

Chama hicho kiliamua kuingia barabarani kuandamana baada ya kikao cha Kamati Kuu yake kuazimia kufanywa kwa maandamano hayo katika maeneo hayo.

Licha ya kutamatika kwa maandamano katika majiji hayo, Mbowe alisisitiza maandamano ndiyo utakaokuwa utaratibu mpya wa chama hicho kuwasilisha hoja zake dhidi ya Serikali.

Mbowe ametoa kauli hiyo jijini Arusha leo Jumanne, Februari 27, alipohutubia umati wa wananchi baada ya kuhitimisha matembezi ya maandamano yaliyoanzia maeneo mbalimbali mkoani humo.

Mwanasiasa huyo amesema kesho wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wa juu wa chama hicho wanatarajia kwenda Mtwara.

Safari hiyo, amesema itafuatiwa na vikao vitakavyoanza wiki ijayo na kufanyika kwa wiki nzima ndani ya mkoa huo na kwamba huko ndiko litakapotengenezwa Azimio la Mtwara.

“Tunapomaliza mkutano wetu wa leo, kesho  tunaondoka wote tunakutana Mtwara, wiki ijayo tutakutana Mtwara kwa wiki nzima. Kamati Kuu ya chama chetu na watendaji wakuu wa chama chetu, tunakwenda kutengeneza Azimio la Mtwara. Tukimaliza Mtwara tutalitangazia Taifa hatua zinazofuata,” alieleza Mbowe.

Hata hivyo, amesema kilichochagiza chama hicho kuingia barabarani kuandamana,  ni kile walichokiona kwamba CCM haijaonyesha nia ya mabadiliko ya sheria zozote.

Ameeleza hadi sasa wametembea jumla ya kilomita 169 katika maandamano yaliyofanyika Dar es Salaam (Januari 24), Mwanza (Februari 15), Mbeya (Februari 20) na jana jijini Arusha.

Ndiyo utaratibu wetu

Ameeleza kuanzia sasa maandamano ndiyo utakaokuwa utamaduni wa maisha ya chama hicho hadi pale kitakapoona yanapatikana mabadiliko ya kweli nchini.

“Tunapoandamana kwa kilomita 20 ni kielelezo tosha cha ujenzi wa hisia. Huko nyuma CCM walisema Watanzania hawapendi kuandamana ni uongo,” amesema.

Kwa mujibu wa Mbowe, maandamano yanalenga kupeleka ujumbe kwa watawala kwamba kinachozungumzwa na viongozi wa vyama vya upinzani ni kwa niaba ya Watanzania wengi.

Amesema maandamano hayo yanalenga kuwafanya watawala watambue Chadema kinawakilisha wananchi wengi wenye maumivu na wasio na furaha katika nchi yao.

“Tunaandamana ili kuonyesha kwamba tuko tayari kuumia ili kurekebisha,” amesema.

Alipopata fursa ya kuhutubia wananchi, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, amedokeza vikwazo vilivyowekwa hadi kufanikishwa kwa maandamano hayo.

Miongoni mwa vikwazo hivyo, amesema ni bodaboda kulipwa ili wasishiriki maandamano, lakini walishiriki kwa kuwa wana mapenzi na Chadema.

“Walikuwa na nia ya kuzuia watu wasije kwenye maandamano, wameshindwa,” amesema Lema akisisitiza ‘Arusha ni ya Lema’ na kuwashukuru wote waliojitokeza kuwa wana mapenzi mema

"Hii ndio maana umeona kwenye maandamano yetu leo  licha ya mvua kubwa kunyesha lakini hawakurudi nyuma kwenye maandamano. Hii ni kutokana na hasira na ugumu wa maisha uliosababishwa na upandaji holela wa bidhaa mbalimbali," amesema Lema 

Maandamano yalivyokuwa

Kama ilivyokuwa katika maandamano ya awali, viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho waligawanyika katika makundi matatu, Lissu aliongoza kundi lake, Mbowe alikuwa na lake na Godbles Lema alikuwa na la kwake.

Mvua kubwa iliyonyesha haikuwa kikwazo cha maandamano hayo, kwani waandamanaji waliendelea na matembezi hayo na walionekana kuserebuka katikati ya mvua hizo.

Walianza asubuhi hadi mchana walipofika kwenye viwanja vya Reli kulipofanyika mkutano wa hadhara. Maandamano hayo yalisababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli ikiwemo watumiaji wengine wa barabara kushindwa kupita.

Katika msafara ulioongozwa na Lissu walikuwepo pia wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, John Heche, Peter Msigwa na Spika wa Bunge la Wananchi la chama hicho, Suzan Lyimo.

Msafara huo ulishereheshwa na wimbo wa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Blad Key ‘Vinapanda Bei’ uliokuwa ukisikika ukipigwa huku waandamanaji wakiendelea na safari.