Baada ya kuukosa urais mara tano, Odinga kutoa hatima yake leo

Aliyekuwa mgombea wa Azimio la Umoja kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022, Raila Odinga

Muktasari:

  • Aliyekuwa mgombea wa Azimio la Umoja kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022, Raila Odinga leo Agosti 16,2022 saa 8 mchana anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari juu ya kilichotokea katika uchaguzi huo.

Nairobi. Aliyekuwa mgombea wa Azimio la Umoja kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022, Raila Odinga leo Agosti 16,2022 saa 8 mchana anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari juu ya kilichotokea katika uchaguzi huo.

Macho na masikio ya watu wengi ndani nan je ya nchi yataelekezwa kwa mwanasiasa huto kwa kuwa baada ya kambi yake kukataa kutambua matokeo yaliyompa ushindi Dk William Ruto ambaye alipata kura milioni 7.1 (asilimia 50.49) dhidi ya kura milioni 6.9 (asilimia 48.85) alizopata Odinga.

Wagombea wengine kwenye uchaguzi huo ni George Wajackoyah aliyepata kura 61,969 (asilimia 0. 44) na David Waihiga alipata kura 31,987 (asilimia 0.23).

Odinga amegombea urais wa Kenya mara tano ikiwamo uchaguzi uliofanyika Agosti 9 mwaka huu na mara zote alizogombea alishindwa na wapinzani wake.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa vyombo vya habari wa kampeni za Azimio la Umoja, Dennis Onsarigo kupitia ukurasa wake wa twitter ambapo amesema Waziri Mkuu mstaafu huyo atahutubia kwenye eneo la KICC, kituo cha vyombo vya habari.

Odinga atazungumza leo zikiwa zimebaki siku 6 za kikatiba kwa mgombea yeyote ambaye hajaridhika na matokeo kwenda kufungua mashtaka mahakamani.