Mwili wa msimamizi wa uchaguzi Kenya aliyetoweka wapatikana porini

Mwili wa msimamizi wa uchaguzi Kenya aliyetoweka wapatikana porini

Muktasari:

Saa chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya kumtangaze Dk William Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya, mwili wa ofisa wa tume hiyo aliyepotea akiwa kituo cha kupigia kura umepatikana katika msitu wa Kilombero akiwa amefariki.

Nairobi. Saa chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya kumtangaze Dk William Ruto kuwa Rais mteule wa Kenya, mwili wa ofisa wa tume hiyo aliyepotea akiwa kituo cha kupigia kura umepatikana katika msitu wa Kilombero akiwa amefariki.

Ofisa huyo Daniel Musyoka (53), alikuwa msimamizi wa Kaunti ya Embakasi Mashariki iliyopo katika jiji la Nairobi na mwili wake umepatikana jana, Jumatatu Agosti 15, 2022 katika msitu eneo la Kajiado.

Akizungumzia kupatikana kwa mwili huo, Ofisa wa Polisi wa Loitoktok, Kipruto Ruto, amesema walipewa taarifa za kuwapo kwa mwili huo ambao baadaye dada zake waliutambua mwili huo ni wa ndugu yao.

Ruto amewataja dada walioutambua mwili wa ndugu yao ni Mary Mwikali na Ann Mboya ambao walikwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Loitokitok na kukiri mwili huo ni ndugu yao.

"Dada zake wawili ndiyo wameutambua mwili huo, sisi tunafanya mawasiliano na makao makuu ya polisi kujua kama mwili huu utapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo Nairobi au utaendelea kubaki katika eneo hilo," amesema Ruto

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, mwili huo ulitupwa katika bondeni karibu na mto ambako ni eneo lenye matukio mengi ya maiti kuokotwa.

Jana Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kabla ya kutangaza mshindi wa kura za urais, alieleza ugumu waliokabiliana nao akitaja pia kuumia, kupotea kwa watumishi wake sambamba na vitisho ambavyo hata hivyo amesema havikuwakatisha tamaa na wametimiza majukumu kikamilifu.