Ruto aahidi kutolipa kisasi, kujenga Taifa

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

Rais mteule wa Kenya, aliyetangazwa muda mfupi uliopita na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, ameahidi hatalipa kisasi kupambana na yoyote aliyekosana naye.

Nairobi. Rais mteule wa Kenya, aliyetangazwa muda mfupi uliopita na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, ameahidi hatalipa kisasi kupambana na yoyote aliyekosana naye.

Ruto ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Agosti 15, 2022 mara baada ya kukabidhi cheti cha ushindi na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati ambaye alimtangaza mshindi kwa kupata kura milioni 7.1 akimshinda mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliyepata kura milioni 6.9

Mwanasiasa huyo amesema hakuna sababu kwa yoyote yule kuwa na wasiwasi kwakuwa yeye ni kiongozi wa Wakenya wote waliomchagua na wasiomchagua.

“Waliotufanyia mambo maovu, wasihofu kwa kuwa hakuna sababu ya kuangalia nyuma, tunaangalia mbele, hakuna sababu ya kisasi, hili ni Taifa letu, hatuhitaji sababu ya kuanza kunyooshea vidole wala kugawana maeneo, tuangalie mbele kwa misingi ya kuliendeleza Taifa letu”.

Ruto pia ameahidi kufanya kazi na wapinzani kwa kiwango kinachostahili kwa kuwa wao ndiyo jicho la utendaji wa serikali

“Hatuwezi wote kuwepo uongozini, nitaongoza serikali kwa uwazi na kushirikiana na upinzani kwa kiwango cha kutosha katika kuangalia utendaji wetu”

Mwanasiasa huyo pia, amemshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kufanya naye kazi kwa miaka 10 katika mazingira mbalimbali na ataendeleza msingi imara unaoachwa na kiongozi huyo kwa faida ya Wakenya.

Matokeo ya urais kwa wagombea wote kwa asilimia ni kama ifuatavyo;


William Ruto-50.49 %


Raila Odinga- 48.85 %


David Waihiga- 0.23 %


George Wajackoyah-0. 44