Baba adaiwa kumbaka mwanaye wa miaka minne

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo

Muktasari:

  • Baba ambaka mtoto wa kumzaa baada ya kutengana na mkewe

Geita. Ukistaajabu ya Musa utaona ya firauni. Hii ni baada ya baba mmoja mkazi wa Mwembeni kata ya Nyankumbu mjini Geita kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka minne.

Tukio hilo limetokea Jumamosi ambapo baba wa mtoto huyo anadaiwa kutenda kosa hilo baada ya kugombana na mkewe, kisha mkewe kuondoka na kumuachia watoto.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea tukio hilo na kudai iligundulika baada ya mtoto huyo akiwa anacheza na watoto wenzake kujishika kila mara sehemu za siri.

“Mtoto huyu alipoonekana hayuko sawa hasa sehemu za siri jirani alimuangalia na kuona ameingiliwa, akapelekwa hospitali na imethibitika alibakwa,”amesema Kamanda Mwabulambo.

Kamanda Mwabulambo amewataka wanawake kuwa walinzi wa kwanza wa watoto wao hasa kunapotokea migongano ya kifamilia ili kuepusha watoto kuingia kwenye matatizo kama hayo.

Akizungumza na gazeti hili mama wa mtoto huyo (jina tunalo) amesema taarifa za mwanaye kubakwa alizipata kutoka kwa mumewe baada ya kumpigia simu akitaka kuja kuwatazama watoto baada ya yeye kukamatwa akituhumiwa kumbaka mwanaye.

“Alinipigia simu akidai nije kumuona mtoto anasingiziwa kubaka akidai labda kabakwa na watoto wenzake nikamwambia aache kuwasingizia watoto wa watu kwa sababu hadi mimi naondoka tulikua tukigombana tabia yake ya kutaka kulala anapolala mtoto huyo kila anaporudi nyumbani amelewa.

“Mume wangu ni mlevi sana na kila alipokuwa akirudi amelewa hung’ang’ania kulala anapolala mtoto huyo, ukimzuia anakupiga hata siku naondoka na kumuacha na watoto alinipiga kisa amelazimisha kulala kwenye kochi alilolala mdogo wangu nilipomzuia ndipo akanipiga na kutufungia nje,” amesema.

Majirani wa familia hiyo Fikiri Paulo na Fadhila Abdalah wamesema tatizo kubwa la baba huyo ni ulevi na pindi anapokuwa mlevi huwa mkorofi na asiyesikiliza ushauri.