Baba watoto njiti agoma kuchukua miili

Tabora/Dar. Licha ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kwa watoto njiti waliofariki dunia wilayani Kaliua Mkoa wa Tabora, baba wa watoto hao, Issaka Raphael amegoma kuchukua miili akitaka watuhumiwa wa tukio hilo wakamatwe kwanza.

Mei 9 mwaka huu katika kituo cha afya Kaliua, Musaneza Benson (25) alijifungua pacha waliodaiwa kufariki muda mfupi baadaye na siku iliyofuata maiti moja ilikutwa imenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili.

Awali, mzazi huyo aliambiwa na wahusika wa Hospitali ya Wilaya ya Urambo kuichukua miili ya watoto wake baada ya kufanyika uchunguzi uliohusisha wanandugu wanne, polisi watatu kutoka wilayani Kaliua, daktari mmoja na mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti.

Akizungumza na Mwananchi jana, baba huyo alisema, “nimekataa kuichukua kwa vile wahusika wanaofahamika bado hawajakamatwa, bali wamesimamishwa kazi tu.”

Alipoulizwa baada ya kukataa kuichukua miili aliambiwaje, alisema kuwa itabidi agharamie malipo ya kuihifadhi katika hospitali hiyo mpaka pale watuhumiwa watakapotiwa nguvuni.

Mzazi huyo alieleza katika uchunguzi huo, alishirikiana na kaka zake wawili na mmoja wa watoto wa kaka yake na kubaini mtoto mmoja mwili wake aliyemtaja kwa jina la Kulwa kuwa sawa, isipokuwa Doto ambaye mwili wake ulikutwa na kasoro kadhaa.

Alizitaja kasoro hizo ni sehemu ya uso wake ngozi kuondolewa, jicho kutokuwepo pamoja na shimo kwenye paji la uso, huku sehemu ya pua yake ikiwa imekatwa.

Kutokana na taarifa hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Angellah Kairuki alisema amewasimamisha kazi wauguzi wawili wa kituo hicho cha afya ili kupisha uchunguzi na amekabidhi kwa Jeshi la Polisi suala hilo ili waendelee na uchunguzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi alisema kukataa kuchukua miili hiyo si busara, kwani ni kushindwa kutenda haki kwa viumbe hao.

“Jeshi la Polisi lina utaratibu wa kufanya kazi na kwa sababu hiyo hawezi kushinikiza, lazima watu wakamatwe hata bila kujulikana kwa uwazi.”

Kauli ya wanataaluma

Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Alexander Baluhya alisema mama anapojifungua watoto kabla ya umri wa mimba kukamilika, mwongozo unawataka watumishi wa afya kuwafikisha kituo kingine cha rufaa kwa matibabu zaidi.

“Utaratibu ni muda huohuo wapelekwe kwa haraka, mama apewe rufaa kama mfumo unavyoeleza."

Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko alisema katika kituo chochote cha afya, kanuni na mwongozo inategemea na hali ya mgonjwa au watoto waliozaliwa au hali ya mteja ndiyo inaelekeza uharaka wa kuchukua hatua.

Dk Nkoronko alisema si watoto wote wanaozaliwa chini ya wiki 37 au njiti wanatakiwa kukimbizwa kituo kingine kwa haraka, mzazi akijifungua, muuguzi, mkunga au daktari hufanya uchunguzi wa mtoto kwa wakati huo na kubaini hali yake na huweza kupanga vipaumbele.

“Mojawapo ni kumsafirisha mgonjwa haraka wakati akisaidiwa, kuna huduma saidizi za mtoto aliyezaliwa njiti, wengi hupata shida katika mfumo wa hewa, hivyo ni lazima wawasaidie kuendelea kupumua mpaka wafike kwenye kituo cha huduma stahiki,” alisema.