Bajeti ya elimu yagusa rasimu sera mpya, wadau waichambua

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa fedha 2023/24, Bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Wakati Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi na mapendekezo ya bajeti yake ya mwaka wa fedha 2023/2024, rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ni miongoni mwa mambo yaliyotolewa ufafanuzi na wizara hiyo.

Dar es Salaam. Rasimu mpya ya Sera ya Elimu na Mafunzo, ni miongoni mwa mambo yaliyowasilishwa bungeni katika bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo Jumanne Mei 16, 2023 bungeni jijini Dodoma.

Akisoma mapendekezo ya bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2023/2024 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mapitio ya rasimu hiyo yamejikita kuboresha elimu katika ngazi zote nchini.

Ngazi hizo ni pamoja na ile ya awali, msingi, sekondari, ualimu, mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya juu.

“Kwa lengo la kuleta mageuzi ya elimu nchini na kuwapatia wahitimu ujuzi na maarifa stahiki, uhuishaji wa sera unahusisha mabadiliko katika mfumo wa elimu, ili kuwawezesha wahitimu kujiamini, kujiajiri na kuajirika katika mazingira ya utandawazi na hivyo kukidhi mahitaji ya soko,” amesema Mkenda.

Profesa Mkenda, amesema Sera ya elimu toleo la mwaka 2023 limejielekeza katika utoaji wa elimu ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

“Aidha, wizara imefanya mapitio ya mitalaa ili kubaini utoshelevu wake na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya mitalaa kulingana na maelekezo ya Sera,” amesema.

Aidha, Profesa Mkenda amesema wizara inaendelea kupokea maoni kuhusu Sera hiyo hadi Mei 31, 2023 huku Juni 2023 ikijiandaa kuomba idhini ili kuwezesha utekelezaji wake.

Hata hivyo, tangu rasimu ya Sera ya Elimu na Mitalaa itoke kumekuwa na maoni mbalimbali ya wadau ambao kwa namna moja au nyingine wanaonyesha kutoridhishwa na baadhi ya mapendekezo katika rasimu hiyo.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kuwa bado kuna mambo muhimu ambayo hayajazingatiwa ikiwemo kutowatambua maofisa elimu utamaduni, maofisa elimu taaluma, maofisa elimu sekondari na maofisa elimu tehama.

Akizungumza Mei 11, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema licha ya maofisa hao kuwepo kwenye mfumo wa elimu nchini, rasimu ya sera haijazungumzia chochote kuhusu watendaji hao.

Vilevile, Anna amesema rasimu hiyo haijagusia suala la wasichana waliopata ujauzito wakiwa shuleni kuruhusiwa kurudi shuleni baada ya kujifungua.

“Serikali imeruhusu wanafunzi wanaoacha shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kupata nafasi ya kurudi shule baada ya kujifungua, rasimu ya sera ya elimu haionyeshi hilo, hii inatupa wasiwasi,” amesema Anna.

Kwa upande wake, Geofrey Mlwilo muhitimu wa Chuo Kikuu amepongeza uwepo wa lugha ya kiingereza katika kufundishia huku akishauri kurudishwa kwa mitihani kwa wanaomaliza shule ya msingi ili kulinda ubora wa elimu.

“Katika matumizi ya kiingereza kwa shule za sekondari nimependa kwasababu itaendelea kutuweka katika ushindani wa soko la dunia kwa sababu lugha hiyo ni ya kimataifa.

“Unavyozungumzia kuondoa baadhi ya mitihani naona kama itaathiri ubora ya elimu yetu maana tutakuwa na wanafunzi wengi sekondari ambao hawana uwezo kwasababu walipita bila kupimwa,”amesema Mlwilo.

Mapendekezo muhimu ya rasimu

Rasimu ya Sera ya Elimu inayopendekezwa sasa itaenda kuchukua nafasi ya Sera ya elimu ya mwaka 2014 ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wadau wengi kwa madai kwamba haiendani na mabadiliko ya Tehama na utandawazi.

Katika rasimu ya toleo la mwaka 2023 baadhi ya mambo ya muhimu yanayopendekezwa ni pamoja na; elimu ya msingi itakuwa ya lazima na itaanza darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Pia, miaka ya kusoma elimu ya msingi kuwa miaka sita badala ya saba, huku elimu ya awali ikiwa mwaka mmoja, kuanza kazi kwa Bodi ya Usajili wa Waalimu, kufutwa kwa ualimu wa cheti na sasa wataanzia ngazi ya stashahada.

Jambo lingine ni ongezeko la lugha za kigeni ambapo shule zitakuwa na uchaguzi wa kufundisha Kiarabu, Kifaransa na Kichina huku lugha ya kiingereza ikianza kufundishwa darasa la kwanza.

Aidha akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo, profesa Mkenda ameliomba Bunge kuidhinisha Sh1.67 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikilinganishwa na Sh1.02 trilioni iliyotengwa mwaka wa fedha 2022/2023.