Bajeti ya Sh63.5 bilioni kukamilisha miradi viporo Mufindi

Muktasari:

Bajeti hiyo pia,  itatekeleza  shughuli mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa

Mufindi.  Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa, wamesema bajeti ya Sh63.5 bilioni iliyopitishwa itaenda kukamilisha miradi viporo ambayo hajakamilika.

Bajeti hiyo pia,  itatekeleza  shughuli mbalimbali za katika halmashauri hiyo.

Akizungumza na Mwananchi  leo Januari 31, 2024 baada ya kumaliza mkutano wa baraza maalumu la rasimu ya mapendekezo ya bajeti, diwani wa viti maalumu wa Tarafa ya Kasanga Asunta  Mtende amesema maboma mengi  yalikuwa bado hayaisha, hivyo kupitia bajeti hiyo baadhi ya maboma hayo yatamalizwa.

"Tumejipanga kupunguza kwa kiasi kikubwa umaliziaji wa maboma, ndio maana tumepitisha bajeti hii,"amesema Mtende.

Diwani wa Mtwango, Monte Kilamlya amesema bajeti hiyo itaenda kusaidia kwa kiasi fulani kumaliza miradi viporo iliyoanzishwa na wananchi.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  Clemence Bakuli amesema madiwani hao wanatakiwa kupitisha bajeti kwa kuzingatia mahitaji ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho kutokana na ahadi iliyotoa kwa wananchi.

Pia, amesema chama kimetoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali kuhakikisha hakuna mapato yatakayopotea kwa sababu wamepitisha bajeti na vifungu hivyo, lakini bado kuna mianya  inayovujisha mapato hayo.

Awali, akizungumza kabla ya kuhitimishwa baraza hilo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Festo Mgina amesema wamepitisha bajeti hiyo lakini jitihada za makusudi zinahitajika ili kufikia malengo hayo hasa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

" Jambo la ukusanyaji wa mapato linahitaji ushirikiano kwa madiwani pamoja na timu ya mkurugenzi  kwa sababu asilimia 87 tunategemea mazao ya misitu, lakini kumekuwepo na baadhi ya watu wanaotorosha mazao hayo,"amesema Mgina.

Amesema kazi kubwa iliyopo kwao ni kuhakikisha wanawatendea haki wananchi ambao wamewachagua kwa kutekeleza yaliyomo kwenye ilani ambayo chama kilisema ndio matarajio ya wananchi.

"Matarajio ya wananchi ni kuona miradi mbalimbali inatekelezwa ikiwamo ujenzi wa madarasa, zahanati na vituo shikizi, hivyo ni muhimu sana kuhakikisha mapato ya ndani yanakusanywa ili kuweza kutekeleza mahitaji hayo ya wananchi katika maeneo yetu,”amesema Mgina.