Bakwata kumwandalia dua maalumu Mzee Mwinyi

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dk Abubakar Zuber akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  leo Machi 7, 2024 alipokuwa akitoa salamu kwa waislamu wote kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhan. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, ameelezea nia ya dua hiyo na kumuenzi Mwinyi kwa mchango wake kwa Waislamu na taifa kwa ujumla.

Dar es Salaam. Wakati Taifa leo likihitimisha siku ya saba za maombolezo ya kifo ch Rais mstaafu, hayati Ali Hassan Mwinyi, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limetangaza kuandaa dua maalumu ya kumuombea kiongozi huyo.

 Mwinyi alifariki Dunia Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam na kuzikwa Machi 2, Mangapwani, Unguja, visiwani Zanzibar.

Akizungumzaa leo Alhamisi, Machi 7,024 ofisini kwake kuhusu mwezi mtukufu wa Ramadhan, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amesema,  “Sisi tutaandaa dua maalumu kwa ajili ya mzee wetu hayati Mwinyi, tutaeleza mambo mengi aliyoyafanya na mchango wake kwa waislamu na y yale aliyotuachia. Alikuwa ni mwalimu na mtu mwenye hekima,” amesema Sheikh Zuber.

Kuhusu mwezi mtukufu wa Ramadhan, Sheikh Zuber amewataka wafanyabiashara kutoficha bidhaa au kupandisha bei na kuufanya kuwa mwezi wa kujipatia kipato.

 “Niwaase wafanyabiasha kutoufanya mwezi mtukufu wa Ramadhan kuwa wa kujipatia kipato, kufanya hivyo ni kujitafutia laana, hamtapata baraka kwa kuwatesa wanaofunga,” amesema.

Mara nyingi kipindi cha mfungo wa Ramadhan, baadhi ya wafanyabiashara hupandisha bei ya bidhaa mbalimbali hasa za vyakula.

Waislamu wanatarajia kuanza kufunga Machi 11, 2024 kutegemea muandamo wa mwezi, huku akiwataka watakaouona kutoa taarifa Bakwata au kamati ya mwezi.

 “Jumatatu ni mwezi 29 ambao kiutaratibu ndio mwezi wa mfungo, waislamu popote mlipo atakayeuona atoe taarifa kwa mamati ya mwezi, ili tuweze kutangaza,” amesema.