Balozi Chana aipa kazi Bodi mpya Ngorongoro

Muktasari:
- Waziri wa Maliasili na Utalii amezindua Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro akiitaka kusimamia mikakati ya kuongeza watalii na mapato ya Serikali katika sekta hiyo.
Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, akiwataka kusimamia kikamilifu mamlaka na kuongeza maeneo mapya ya uwekezaji ili kuongeza pato la Taifa.
Balozi Chana ameyasema hayo Septemba 28 wakati akizundua bodi hiyo jijini Arusha, akiitaka kusimamia ipasavyo shughuli za mamlaka hiyo sambamba na kuweka mikakati mipya itakayosaidia mamlaka hiyo kuendelea kukua zaidi.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuongeza watalii hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025, hivyo waweke mikakati zaidi kuhakikisha wanafikia malengo hayo.
Dk Chana amesema kuwa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hivi sasa inachangia asilimia 17 ya mapato ya utalii, hivyo ijizatiti kuvuka malengo.
"Tuchukue mfano kwa mwaka 2019/20 kabla ya mlipuko wa Uviko 19, eneo la Mamlaka lilitembelewa na zaidi ya wageni 700,000 na kupata mapato ya Sh123 bilioni.
“Kutokana na changamoto ya Uviko19 idadi ya wageni ilishuka hadi kufikia wageni 191,000 na kupata mapato ya Sh31.4 bilioni kwa kipindi cha mwaka 2020/21," amesema Dk Chana.
Amesema baada ya Serikali kutangaza vivutio kupitia filamu ya Royal Tour iliyotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wageni wameongezeka kufikia 425,000 na mapato ya kufikia Sh91.1 bilioni kwa mwaka 2021/22.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo amesema, watahakikisha wanafanya kazi kwa uaminifu na kuhakikisha mamlaka hiyo inakuwa bora kimataifa.
Amesema kuwa, watahakikisha wanahamasisha watalii wa ndani kutembelea mamlaka hiyo huku wakiahidi kufikia malengo yaliyowekwa ya kufikia idadi ya milioni tano.
"Tutahakikisha tuna buni mazao mapya ya utalii na tunaahidi kusimamia kwa ufanisi uhamishaji wa wananachi kuhamia kijiji cha Msomera na tutafanya zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa ili azma ya wizara iliyopangwa itimie," amesema Jenerali Mabeyo.
Naye Msajili wa Hazina Benedicto Mgonya amesema kuwa, bodi ya wakurugenzi ndo chombo kinachoongoza hivyo amewataka kuwa na mfumo madhubuti katika kuhakikisha mamlaka hiyo inazidi kuimarika.
Aidha, amewataka kusimamia mamlaka hiyo kwa kuzingatia sheria na miongozo inayotolewa na kutoa taarifa za utendaji wake na kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi katika utendaji kazi na kufikia malengo mbalimbali yaliyowekwa.