Balozi Polepole ahamishiwa Cuba
Balozi Humphrey Polepole anayeiwakilisha Tanzania nchini Cuba.
Muktasari:
- Rais Samia amefanya uteuzi na Balozi mmoja na kufanya mabadiliko ya vituo kwa kwa mabalozi wawili akiwemo Polepole aliyehamishiwa nchini Cuba.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Balozi mmoja na kufanya mabadiliko ya vituo kwa mabalozi wawili akiwemo Balozi Humphrey Polepole kuiwakilisha Tanzania nchini Cuba.
Polepole ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM, mstaafu, kabla ya uteuzi huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Polepole aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa, kabla ya kuteuliwa kuwa kuwa Balozi nchini, Malawi amedumu kwa mwaka mmoja tangu alipoteuliwa Machi 15, 2022 na kuhamishwa kituo.
Katika uteuzi huo Balozi Luteni Jenerali mstaafu, Yacoub Mohamed kuiwakilisha Tanzania katika Falme za kiarabu (UAE) na kabla ya uteuzi huo alikuwa Balozi nchini Uturuki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, amesema Rais Samia amemteua Idd Self Bakari kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki.
Kabla ya uteuzi huo Balozi Bakari alikuwa Konseli nchini Mkuu nchini Dubai.
“Tarehe ya uapisho kwa Balozi Bakari itatangazwa baadaye,” imesema taarifa hiyo.