Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bandari bado kizungumkuti

Dar/Dodoma. Sakata la makubaliano ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai katika uendeshaji wa bandari nchini bado ni kizungumkuti na limeendelea kuibua mijadala nchini, hasa mitandaoni.

Mijadala hiyo inaibuka wakati Bunge kupitia kwa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) likipokea maoni ya kuridhia makubaliano hayo yanayoelezwa na Serikali kuwa yatachochea ufanisi wa huduma mara utekelezaji utakapoanza.

Wakati hayo yakiendelea, mkataba wa makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai umesambaa mitandaoni na mmoja wa vigogo wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi alilieleza gazeti hili kuwa “ni wa kweli lakini sijajua umefikaje huko mitandaoni.”

Makubaliano ya awali yaliingiwa Februari 28 mwaka jana kati ya Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Duban Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.

Wakati sintofahamu ikiendelea, macho na masikio jana yaliekelezwa jijini Dodoma kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliyekuwa amewaita waandishi wa habari jana asubuhi ikitarajiwa ungetolewa ufafanuzi.

Ingawa haikuelezwa waziri huyo alikuwa anakusudia kuzungumzia nini, lakini waandishi waliokuwepo walikuwa wakitaka ufafanuzi wa maeneo kadhaa yanayosambaa mitandaoni kuhusu uwekezaji huo, kabla ya mkutano huo kuahirishwa hadi siku nyingine.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa hakuwa tayari kuzungumzia mkataba huo wa makubaliano alipotafutwa na Mwananchi, bali aliwaomba Watanzania kupuuza baadhi ya taarifa za mitandaoni, ikiwemo ya uwekezaji huo kuchukua miaka 100.

“Huo ni uongo, kwani hakuna sehemu yoyote ambayo imeeleza ukomo huu wa muda,” alisisitiza.

Mbossa alisema mpaka sasa hakuna mkataba wowote wa utekelezaji ulioingiwa, bali kilichofanyika ni makubaliano ya ushirikiano na ndicho kimepelekwa bungeni kama ambavyo Katiba inaelekeza.

“Tukijadili sasa, tutakubaliana maeneo ya uwekezaji na utakuwa wa miaka mingapi, hiki bado hakijafanyika. Hivyo Watanzania wawe na subra, kwani wanachokwenda kukifanya kina masilahi makubwa kwa Taifa,” alisema Mbossa.

Wakati Mbossa akieleza hayo, mchambuzi huru wa mikataba ya kimataifa ya biashara na uwekezaji, Roselian Jackson alisema wasiwasi wa wananchi unatokana na majeraha yatokanayo na uzoefu wa changamoto za mikataba iliyowahi kuibua utata nchini.

Jackson alisema ili kujiridhisha katika mikataba ya aina hiyo, Serikali inalazimika kujiridhisha kwanza na mwekezaji kuhusu uwezo, uzoefu, usajili na mwenendo wake katika utoaji huduma.

“Hili ni eneo muhimu kuliko yote kabla hata ya kuutazama mkataba wenyewe, hofu ya kuhoji mwekezaji ni nzuri na Serikali inatakiwa kuwaondoa hofu wananchi,” alisema Jackson.

Jackson alisema baada ya kuondoa hofu hiyo, hofu ya pili inahusisha makubaliano ya mkataba wenyewe ambao haujaingiwa rasmi na Serikali. “Tusubiri mkataba utakapoandaliwa na inabidi kila Mtanzania apate haki hiyo ya kujulishwa namna gani Taifa litanufaika.”
 

Zitto: Ni hatua nzuri

Kutokana na kinachoendelea, gazeti hili lilizungumza na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema “tumelisikia suala hili, ninapitia nyaraka zote muhimu ili tuweze kutoa maoni yenye hakika.”

Zitto, aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) alisema, “nimekaa bungeni miaka 15, sikumbuki hata mara moja Serikali kutaka ridhaa ya Bunge kuingia mikataba ya kibiashara. Wabunge wazingatie masilahi ya taifa.”

Alisema mara zote Serikali ilisaini mikataba juu kwa juu bila kuzingatia masharti ya Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, kwa maana hiyo, “Bunge likipitisha azimio ndiyo majadiliano ya mkataba yanaanza. Ni hatua nzuri sana. Sasa Bunge lifanye kazi yake.”

Kifungu hicho cha Katiba kinaeleza, “kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.”
Zitto, ambaye kitaaluma ni mchumi alisema, “nimemsikia Waziri wa Nishati (January Makamba) akitamka mkataba wa LNG Lindi (HGA) utajadiliwa na Baraza la Mawaziri na kisha kuidhinishwa na Bunge.

“Sasa naona mjadala kuhusu mkataba wa uendeshaji wa Bandari za Tanzania kwamba Bunge linaombwa kwanza ruhusa. Ni hatua kubwa. Miaka yetu tukiwa bungeni tulikuwa tunasikia tu mikataba inasainiwa mahotelini kwa siri,” alisema.
 

Mbowe alonga

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa ziarani Italia alitoa tamko la awali la chama hicho kuhusu suala hilo akisema “mkataba huo una viashiria vyote vya kuhatarisha usalama wa nchi kiuchumi na kisiasa.

“Hivyo, kwa hatua ya sasa, ninamtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa azimio hili bungeni kwa dharura ili kupisha mashauriano ya muafaka wa kitaifa juu ya jambo hili nyeti. Lakini mheshimiwa Rais unaruhusu vipi suala hili kupelekwa bungeni kwa uharaka wote huu,” alihoji Mbowe.

Mbowe aliwataka wawakilishi wa wananchi kutopitisha azimio hilo hadi uwepo uelewa wa pamoja, kwani kupitisha kwao ni kuruhusu michakato mingine kuendelea.

Mbowe alisema makubaliano yanaonyesha, “unaendelezwa utamaduni wa kuwapa wawekezaji wa nje manufaa makubwa ya kikodi na faida nyingine, ambao umesababisha taifa letu kupoteza utajiri na rasilimali zake asilia, kama vile madini, bila kupata manufaa yoyote ya maana.” “Chini ya mkataba huu, misamaha ya kodi na manufaa mengine kwa DP World yamewekewa ulinzi uleule wa kutobadilishwa wakati wa kipindi chote cha mkataba, kama ilivyokuwa kwenye madini na sekta nyingine za uchumi wetu,” alisema.

“Zaidi ya ahadi za jumla jumla za manufaa kwa nchi yetu, mkataba huu hauonyeshi manufaa ya waziwazi kwa nchi yetu na kwa uchumi wetu.”

Mbowe alisema mara baada ya yeye pamoja na viongozi wenzake, Tundu Lissu (Makamu wake-Bara) na John Mnyika (Katibu Mkuu) watakaporejea nchini, watalijadili suala hilo kwa kina na kutoka na msimamo madhubuti.

“Bandari ni chanzo kikubwa cha mapato na sisi Chadema hatupingi uwekezaji, lakini tunataka uwekezaji ambao ni rafiki, wenye uwazi,” alisema.

Mwezi uliopita, Mbunge wa Kilombero (CCM), Abubakar Asenga akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2023/24 aligusia uwekezaji huo akisema, “bandari haiuzwi, haibinafsishwi (bali) tunaingia mashirikiano ya uendeshaji.”

Asenga alisema, “hawa DP Word wamewekeza nchi saba Afrika zenye bandari, duniani wana bandari 70, hapa tunafanya siasa siasa, nusu ya bajeti tunaikosa. Ukienda huku unamkuta huyu, ukienda bandarini mfanyabiashara anamchafua mwingine.”

Kulingana na vyanzo vyetu, lengo la makubaliano ni kuweka utaratibu wa kisheria wa maeneo ya ushirikiano kwa ajili ya kuendeleza, kuboresha na kuendesha bandari za kwenye bahari, maziwa, maeneo maalumu ya kiuchumi na miundombinu inayoendana na shughuli za bandari nchini.

Maeneo ya ushirikiano yanalenga kujumuisha kujenga uwezo, kuhamisha ujuzi, teknolojia na utaalamu, kuimarisha vyuo vya mafunzo na intelijensia za masoko.
Jumatatu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alinukuliwa na gazeti dada la The Citizen kwamba, kampuni ya DP World ni sahihi kwa Tanzania na italeta tija.

Mbarawa alisema kampuni hiyo itaongeza chachu ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 233.7 katika kipindi cha miaka kumi ijayo katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia ufanisi wa huduma.

Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maeneo ya maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Profesa Mbarawa alisisitiza kampuni hiyo ina nafasi ya kipekee ya kushirikiana na Serikali kwa kuwa ni kampuni ya kimataifa ya usafirishaji yenye uwezo wa kuleta mabadiliko yanayohitajika nchini katika mnyororo mzima wa thamani wa vifaa.

Alisema kampuni hiyo ina rekodi ya kimataifa ya kusimamia, kuendesha na kuwekeza katika miundombinu ya biashara barani Afrika kwa zaidi ya miaka 20 kwa viwango vya juu zaidi vya kimataifa.

“Tuna imani kubwa na DP World na tunapanga kuipa nafasi tano hadi saba kushughulikia. Tukiwa na DP World, tunatarajia kuona uboreshaji wa utendaji wa bandari. Tunatarajia kuona muda wa uondoaji wa meli ukipunguzwa hadi siku moja kutoka nne hadi tano za sasa,” alisema Profesa Mbarawa.