Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baridi, barafu inavyobadili mfumo wa maisha Makete


Muktasari:

  • Kama sio mafua makali, kifua kikavu basi vichomi ni kati ya magonjwa yanayowasumbua wakazi wengi wa mikoa ya nyanda za juu kusini kutokana na baridi kali.

Nyanda za Juu Kusini. Kama sio mafua makali, kifua kikavu basi vichomi ni kati ya magonjwa yanayowasumbua wakazi wengi wa mikoa ya nyanda za juu kusini kutokana na baridi kali.

Na si rahisi katika kipindi hiki kukutana na mtu ambaye hajavaa vazi zito la kujikinga na hali ya hewa iliyopo hivi sasa.

Kwenye baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Njombe na hususan Wilayani Makete, barafu inaanguka mithili ya ile iliyozoeleka kwenye nchi za Bara la Ulaya.

Uotaji moto wa mkaa kwenye majiko ni moja ya njia wanazotumia wakazi wa mikoa hiyo kujikinga na baridi hata hivyo, bado baadhi yao wanalalamika matumizi makubwa ya mkaa.

Limekuwa jambo la kawaida kwa wakazi wa Mkoa wa Njombe kumaliza siku nzima bila kuona jua zaidi ya ukungu na hali ya giza linaloambatana na manyumnyu ya mvua.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Waziri Kindamba akizungumza na Mwananchi juzi juu ya hali ya hewa hiyo, alisema pia ni fursa kwa Watanzania wanaoishi kwenye mikoa ya joto kwenda Njombe kushuhudia namna barafu inavyoshuka kama ambavyo imekuwa ikionekana katika nchi mbalimbali barani ulaya.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusambaa kwa picha zinazoonyesha hali ilivyo, Waziri alisema baridi kali ni miongoni mwa neema ambazo mkoa wa Njombe umejaliwa.

“Tumezungumza na wenzangu wa sekretariati ya mkoa kwa ajili ya kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye michezo ya barafu ili watu waweze kucheza katika miezi hii ambayo barafu ni kubwa,” alisema Kindamba.

Aliwataka wazazi kuendelea kuwalinda watoto hasa kipindi hiki ambacho baridi ni kali kwa kuwavisha nguo za kutosha ili kuwakinga watoto.

Awali, Ofisa mfawidhi wa kituo cha hali ya hewa kilichopo Igeli kata ya Luponde mkoani Njombe, Joseph Fumbo alisema ni kawaida kipindi hiki kuwa na baridi kali mkoani humo.

Aliwataka wakazi wa mkoa huo kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kufuata utaratibu wa kujikinga na baridi.

“Naomba wananchi waepuke kulala na moto wa jiko la mkaa ndani kwakuwa umekuwa ukusababisha vifo” alisema Fumbo.


Simulizi za wananchi

Mkazi wa Kambarage, Njombe mjini, Neema Mgeni alisema kumekuwa na baridi ni kali hasa nyakati za asubuhi na jioni jambo ambalo ni hatari kwa afya.

“Ukiuliza namvalisha mtoto nguo ngapi siwezi kukupatia jibu, hata ziwe kumi ni sawa tu kikubwa nimkinge na barisi kwa sababu amekuwa akibanwa sana na nimonia,” alisema Mgeni na kuongeza;

“Baridi ni kali kiasi kwamba unaweza kunywa chai na usione kama yamoto lakini baadae unakuja kugundua midomo inachubuka kwa kuungua. Inabidi tuzoee ndio kwetu huku,”

Alisema kutokana na barafu, kuna wakati vidole vya mikono huganda mpaka viwekwe kwenye moto na hivyo kushauri walimu waruhusu uotaji wa moto madarasani ili kuwasaidia watoto.


Mkoani Mbeya

Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya walisema baridi imekuwa na athari kubwa kiafya ikiwemo kifua kikavu na mafua makali.

Anitha Mwakagali, mkazi wa Mwanjelwa jijini Mbeya alisema licha ya kuvaa nguo nzito bado baridi imemuathiri.

Baadhi ya wafanyabishara hasa mama ntilie, walisema hali ya biashara kwao ni mbaya kwa kuwa asubuhi na jioni hakuna wateja.

Mama lishe, Janeth Brown alisema kutokana na hali hiyo biashara yake imeyumba tangu mwezi wa sita mwaka huu mpaka sasa.

“Ukipika chakula kinapoa haraka, inabidi muda wote uwe na moto na kama unavyojua bei ya mkaa, huwezi kumudu,” alisema na kuongeza;

“Hali hii inatuathiri licha ya kuwa wabunifu wa kuwasha moto ili kutengeza joto bado ni changamoto sana hususan kwa watoto wa shule ambao tunalazimika kuwavisha nguo nyingi ili wasipate madhara kiafya.”

Mfanyabishara wa makoti ya mitumba, Stephan Ayoub alisema kuwa msimu huu baridi biashara yao kuwa imekuwa ikitegemea wateja katika Mikoa ya Iringa,Makambako na njombe ambako kuna baridi kali tofauti na hapa Mbeya.

“Baridi iliyopo Mbeya ni tofauti na Iringa ,Njombe na Makambako hivyo ndi maneo makubwa tunayotegemea wateja ndio maeneo ambayo biashara ya vileo vikali inafanyika sana,” alisema.

Mkazi wa Milo, Wilaya ya Ludewa, Joel Mhagama alisema; “Baridi ya mwaka huu imekuja tofauti na tulivyotarajia, imedumu kwa mda mrefu lakini pia imekuja na homa ya mafua ya kujirudiarudia. Kwa mfano kwa mda wa wiki tatu zilizo pita kwa hapa Milo hatujabahatika kuliona jua, jua limeanza kuchomoza juzi na Jana,” alisema.

Kwa upande wake, Atilio Mtega kutoka kata ya Lubonde alisema, kuna hali mbili tofauti ndani ya kata yao

“Kwa hapa lubonde imetofautia kwa vijiji, unaweza kutoka Masimbwe jua lina waka na kuna joto lakini ukifika Mkiu wingu limetanda hakuna jua siku nzima, na kwa upande wa barafu sisi huku huwa haidondoki,” alisema.

Vyakula wakati wa baridi

Ofisa Lishe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Pendo Yaleji alisema ili kukabiliana na baridi kali watu wanatakiwa kula vyakula vya joto, kufanya mazoezi na kuvaa nguo zinazotunza joto la mwili.

Alisema kwa kufanya hivyo wengi wanaweza kuepuka magnjwa yanayotokana na mfumo wa hewa ikiwemo Nimonia.

“Vyakula vinavyoweza kuupatia mwili joto vinaweza kuwa suluhisho katika kupambana na baridi,” alisema.