Barrick yatoa ambulance kituo cha afya cha Bugarama

Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold Corporation, Mark Bristow akikabidhi ambulance kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mboni Mhita leo mkoani Shinyanga

Muktasari:

  • Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold Corporation Mark Bristow, amesema Barrick inathamini suala la usalama na afya katika jamii ndiyo maana imeamua kutoa gari hilo.

Shinyanga. Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Barrick, imetoa msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Land Cruiser hardtop, katika Kituo cha afya Bugarama kilichopo kata ya Bugarama Halmashauri ya wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga.

Gari hilo lilikabidhiwa jana na rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold Corporation, Mark Bristow na kupokelewa na Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mboni Mhita.

Akizungumza jana Machi 22 wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya gari hilo iliyofanyika katika Kituo cha Afya Bugarama, Bristow, amesema Barrick inathamini suala la usalama na afya katika jamii ndiyo maana imeamua kutoa gari hilo.

"Gari hili tumelitoa kama sehemu ya mchango wetu kwa jamii ni nje ya Fedha za mfuko wa uwajibikaji kwa jamii, tunaamini litasaidia katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Tutahakikisha tunaendelea kushirikiana na jamii inayozunguka migodi yetu," amesema Bristow.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita ameishukuru Kampuni ya Barrick kwa namna inavyojitahidi kutekeleza miradi mingi inayogusa wananchi huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Wawekezaji ili kuwaletea maendeleo wananchi.

 "Tunawashukuru Barrick kwa kukipatia Ambulance kituo hiki cha Afya cha Bugarama. Gari hili litasaidia kutatua changamoto zilizopo. Nasi tunaahidi kutunza na kutumia gari hili kwa malengo yaliyokusudiwa. Ambulance hii itaongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya," amesema Mhita.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Leonard Mabula na Diwani wa Kata ya Bugarama, Prisca Msoma wameishukuru Barrick kwa kutekeleza kwa wakati ombi la Ambulance ili kutatua changamoto ya huduma za matibabu katika kituo hicho cha afya kinachohudumia jamii ya Bugarama na maeneo ya jirani ikiwemo Geita.

Mganga mkuu wa Halmashauri ya Msalala Dk Sisti Mosha, amesema walitoa ombi la kupatiwa ambulance kutoka Barrick mnamo Januari mwaka huu, hivyo kupatikana kwake kutapunguza changamoto ya usafiri kwa wagonjwa katika kituo hicho cha afya.