Bashe aibua mapya sakata la sukari

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali itaendelea kuwalinda kwa umuhimu wao wafanyabiashara wa sukari nchini, lakini hatakubali wafanyabiashara saba watumie mwanya huo kwa kuwaumiza Watanzania milioni 60.

Dar es Salaam. Sakata la bei ya sukari limeibua mapya baada ya Waziri Kilimo, Hussein Bashe kuonya baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia viongozi wengine wa kisiasa ili kuathiri mwenendo wa bei elekezi ya Sh2, 700 hadi Sh3,200 kwa kilo nchi nzima iliyotangazwa siku tano zilizopita.

 Wakati Mwananchi Digital ikibaini kuendelea kwa changamoto ya bei na kukosekana kwa sukari katika baadhi ya maduka mikoani Dar es Salaam, Bashe amesema hakuna mfanyabiashara yeyote atakayebadili bei hiyo elekezi kwa kushawishi baadhi ya viongozi wakiwamo wabunge.

Bashe aliyeonekana kwenye hali ya kuchukizwa, amesema kokote wanakokwenda na kufanya mazungumzo na viongozi, anapata taarifa zao moja kwa moja. 

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi katika Jengo la Tume ya Umwagiliaji mjini Dodoma jana, Bashe amesema yuko tayari kutii maelekezo ya kubadili msimamo huo kutoka kwa watu wanne pekee na hakuna mwingine kama wafanyabiashara hao wanavyo watumia kushawishi.

“Nchi hii anayeweza kuniambia ondoa bei elekezi wako wanne; Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu. Wako wanne tu. Hawa tu ndio wanaweza kuniita na kunihoji, hakuna mtu mwingine yeyote kuniita na kunihoji,” amesema Bashe kwa msisitizo.

Msingi wa hoja yake unaakisi tangazo la Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) lililotoka katika Gazeti la Serikali kwamba bei hiyo ilianza kutumika Januari 23, kabla ya kukoma Juni 30, 2024.

Kwa tangazo hilo, bei ya chini kwa rejareja ni Sh2,700 na ya juu ni Sh3,200 kutegemeana na maeneo. Wakati bei hiyo elekezi ikitangazwa, baadhi ya mikoa kilo moja ya sukari inauzwa kwa Sh4,000 mpaka Sh6,000.

Baada ya tangazo hilo, baadhi ya wafanyabiashara wamedai bei hiyo haiendani na bei ya kununua, hivyo itawanyonga kibiashara.

Hata hivyo, Waziri Bashe amesema Serikali itaendelea kuwalinda kwa umuhimu wao, lakini hatakubali wafanyabiashara saba watumie mwanya huo kwa kuwaumiza Watanzania milioni 60.

“Nitasimama peke yangu kwa jambo ninaloliamini. Hakuna atakayeniyumbisha. Ninawatahadharisha, ninawaonya. Tumeilinda sekta hii kwa jasho na damu, hatutaruhusu Watanzania milioni 60 wawe mateka wa kampuni saba,” amesema Bashe. 

“Haitawezekana over my dead body (katika maisha yangu). Kwa hiyo ninawaambia, kama wana hoja ya huduma za kubadilisha fedha za kigeni, waje kujadiliana na mimi wizarani.” 

Bashe amesema Serikali ina mfumo wa wazi na unaoeleweka katika bei zilizokuwepo hadi mwishoni mwa Desemba mwaka jana.

“Nimeona niliseme hili kwa umma, waache ku-lobby, wasiponielewa hakuna wasiwasi, nina wakulima wangu 12,000, tutahangaika mwaka mmoja na nusu tu kubadili crop (zao), ni suala la kiuchumi, tunapiga hesabu, je mwananchi anunue sukari Sh6,000 au niruhusu kutoka nje kwa Sh2,000, Sh3,000?.”

Kabla ya kutoa msimamo huo juzi, Bashe alipigiwa simu na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda aliyemtaka kutoa uhakika wa upatikanaji wa sukari kwa bei ya chini wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Bashe aliahidi kuimarisha mfumo wa bei ya soko hilo kabla ya Februari 15, 2024.

Awali, Bashe amesema inawezekana haitoshi kwa kiwango walichotarajia mtaani kutokana na viwanda kusimama uzalishaji.

Hata hivyo, amesema tayari meli ya kwanza imeshafika na itaanza kupakua sukari hiyo kuanzia leo na kesho.

Amesema wanatarajia kuingiza tani zote nchini kufikia mwishoni mwa Februari, mwaka huu.  

“Pili, tutaendelea kufanya tathimini ya hali ya mvua, kuangalia tathimini ya uharibifu wa mashambani kwa sababu hatutaki kuagiza kiwango cha sukari kitakachoua uzalishaji wa ndani. Hatuwezi kutatua suala sukari kisiasa, tutalitatua kwa misingi imara ya sera na suala la mahitaji ya soko na usambazaji,” amesema.