Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bashe atangaza operesheni wavamizi Nanenane

Muktasari:

  • Mawaziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Abdallah Ulega wa Mifugo na Uvuvi wametangaza hatua mbalimbali zinazofanyika ili kuchochea ufanisi wa sekta wanazoziongoza. Marekani yenyewe imepanga kuja na programu ya kudhibiti upotevu wa mazao ya chakula baada ya mavuno.

Dodoma/Dar. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe ametangaza operesheni maalumu ya kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya viwanja vya maonyesho ya wakulima vya Nzuguni (Dodoma) na Mwakangale (Mbeya).

Bashe ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 8, 2024 katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane zilizofanyika Nzuguni jijini Dodoma, huku mgeni rasmi akiwa ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha kimataifa cha Mwakangale cha jijini Mbeya ameshapatikana na watakwenda kubomoa uwanja huo kwa ajili ya kuanza kujenga.

Amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa kushughulikia changamoto ya watu waliovamia katika viwanja vya Nanenane Nzuguni.

“Tumeshawatoa watu wote wamebaki wanane baada ya Nanenane kama utaridhia iende hadi Jumatatu ili watu waendelee kufanya biashara hapa, tutawamalizia wanane waliobaki ili waondoke katika eneo hili,” amesema.

Ombi hilo limeridhiwa na Rais Samia na kusema maonesho hayo yatamalizika Jumamosi hii na Jumapili watu waondoke ili Jumatatu watu wawe makazini.

Bashe amesema operesheni hiyo itakwenda pia Mwakangale mkoani Mbeya kwa kuwaondoa watu wote waliovamia maeneo ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) na Nanenane.

“Hao wote tunaenda kuwaondoa mle ndani kwa sababu ule utaratibu wa kujimilikisha maeneo ya Serikali hasa ya kilimo umefika mwisho,” amesema.

Aidha, Bashe amesema akiwa India na Rais Samia alitaka wawe na vituo jumuishi vya zana za kilimo ambavyo leo amevizindua.

Amesema Rais Samia pia amezindua matreka 500 na power tiller 800 ambazo zitapelekwa kijijini kwa ajili ya wakulima na watawahudumia kwa bei ya ruzuku.

Bashe amesema upatikani wa chakula nchini umefikia asilimia 128 na ukuaji wa sekta ya kilimo umefikia asilimia 4.2.

Amesema malengo waliyopewa na dira ya Taifa na Ilani ya uchaguzi ya CCM, kufika asilimia 130 ya upatikanaji wa chakula na kuwa wanaamini 2024/25 watayafikia malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2025/26.

Waziri huyo amesema lengo lao mwaka ujao, mauzo ya nje ya nchi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 kutoka Dola za Marekani bilioni 2.3 za mwaka uliopita.

Bashe amesema Tanzania ilivyoanza matumizi ya ruzuku ya mbolea, matumizi yalikuwa ni tani 330,000 lakini msimu uliopita wastani wa matumizi ya mbolea ulikuwa ni tani 900,000 za mbolea.


Alichokisema Waziri Ulega

Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya wizara yake kutoka Sh66 bilioni wakati anaingia madarakani hadi kufikia Sh465 bilioni za sasa.

Pia, alitangaza kutoa ruzuku ya asilimia 50 katika chanjo za mifugo nchini katika mwaka 2024/2025 na kutoa bure chanjo ya kuku.

Ulega amesema utoaji wa ruzuku hiyo utafanya bei ya chanjo kupungua ili kuwawezesha wafugaji kumudu kuinunua.

“Tutakuwa tumetoa ruzuku kwa asilimia 50. Wale wafugaji wa ng’ombe na mbuzi itasaidia katika utanuaji wa masoko kimataifa,” amesema Ulega.

Mbali na mifugo mingine, kwa wale wafugaji wa kuku unaweza kusema ni kucheko kwani wao watapewa chanjo bur ili kuwaepusha na hasara ambayo walikuwa wakiipata awali baada ya kuku kufa kwa ugonjwa wa kideri.

Katika mwaka huu wa fedha pia wamepanga kuendelea na programu ya kutoa mikopo nafuu kwa wavuvi ikiwemo boti ambazo zitakuwa 450 na vizimba vya kufugia samaki visivyopungua 900 na vingi vitakuwa kwa ajili ya vijana.

“Leo hii ni ushahidi, kupitia vijana wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT) mifugo, vijana wamepewa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Sh1.1 bilioni na wamepewa vitalu vya kuanzia kazi yao,” amesema Ulega.

Amesema wizara yake pia imejipanga kuendelea kushirikiana na sekta binafsi huku akieleza akifafanua kuwa katika kuboresha ufugaji tayari wanao mradi mkubwa ambao unalenga  kusambaza ng’ombe 17,200 wa maziwa watasambazwa mikoani sambamba na ujenzi wa mabanda ya kisasa 5,000.

Katika kulinda mazingira mifumo ya biogas ili kinamama watakaokuwa wakifuga watumie kinyesi cha mifugo katika kupata nishati safi.


Programu ya Marekani

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle akizungumza kwenye sherehe hizo amesema wanatarajia kuja na programu ya kudhibiti upotevu wa mazao ya chakula baada ya mavuno ambapo Sh53.893 bilioni zinatarajiwa kutolewa katika utekelezaji wake.

Battle amesema anaamini Tanzania inao uwezo wa kuzalisha chakula si tu kwa ajili ya kuilisha Afrika Mashariki bali pia kwa ajili ya kanda nyingine.

“Dhamira ya Serikali ya Marekani ni kuendelea kusaidia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania ndiyo maana tumeongeza pia mchango wetu kutoka Sh296.41 bilioni mwaka 2022 hadi Sh1.13 trlioni mwaka huu,” amesema Battle.

Amesema kama ilivyo kwa wadau wengine, Serikali yake pia inajivunia kuwa miongoni mwa wanaochangia katika sekta ya kilimo kupitia mpango wake wa ‘Feed the future’ ambao unatekelezwa na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

“Kupitia mpango huo wamekuwa wakifanya kazi na wakulima, wafanyabiashara katika kilimo wakilenga kuongeza tija na uzalishaji, kuboresha lishe, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno,” amesema Battle.

“Wakati mafanikio haya yakisherehekewa, Tanzania inao uwezo wa kuzalisha si tu kwa ajili ya kuilisha Afrika Mashari bali kwa ajili ya kanda nyingine.

Pia, amepongeza hatua ya serikali ya kuweka mifumo ya kodi rafiki na inayitabirika huku akisema hatua zaidi zinahitajika “Marekani na wadau wengine tupo tayari kuitangaza Tanzania kwa wawekezaji wa kimataifa na kuwaambia kuwa Nchi ya Tanzania imefunguka kibiashara.