Bashungwa aguswa na upungufu wa maofisa habari

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa ameahidi kushughulikia upungufu wa maofisa habari na mawasiliano katika halmashauri 85 nchini ambazo hazina maofisa hao.

  

Tanga. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa ameahidi kushughulikia upungufu wa maofisa habari na mawasiliano katika halmashauri 85 nchini ambazo hazina maofisa hao.

Hayo ameyasema leo Ijumaa Mei 13, 2022 wakati wa kikao Cha maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini kilichoketi kwa siku tano jijini hapa.

Bashungwa amesema katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara mikoa, minne haina maofisa habari na mawasiliano  na katika halmashauri 184 halmashauri 85 hazina maofisa hao ambao amesisitiza kuwa kisemeo cha Serikali.

“Hili jambo la kutokuwa na maofisa habari kwangu ni kubwa na la muhimu nipambana nalo kuhakikisha tunakuwa na maafisa habari katika halmashauri 85  ambazo hazina.

“Nimatumaini yangu mapacha wangu kaka yangu Nape na Dada yangu Jenista Mhagama wanakubali ili tuweze kusukuma maazimio haya,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu Wizara Ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk Jimmy Yonazi alimuomba Waziri Bashungwa kuwasaidia kushughulikia hiyo changamoto ya kukosekana kwa maafisa habari katika baadhi ya halmashauri na mikoa nchini.

"Tunaomba utusaidie halmashauri zote na zile Taasisi zilizopo katika ofisi Yako zinapata Maafisa habari," amesema Dk Yonazi.

Hata hivyo, kati ya halmashauri 184 ni halmashauri 99 tu ndo zina maafisa Habari na kati ya mikoa 26 ni mikoa 22 pekee ambayo inamaafisa habari .