Bashungwa ahaidi kupambana na rushwa
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza bungeni leo Jumatano Septemba 6, 2023 wakati akijibu maswali ya wabunge.
Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na kuapishwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amejibu maswali ya wabunge na kuahidi kulivalia njuga suala la rushwa.
Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na ameahidi kudhibiti na kupambana na rushwa katika mikataba, manunuzi na usimamizi wa miradi.
Amesema hayo Jumatano Septemba 6, 2023 bugeni wakati alipokuwa akijibu maswali ya wabunge kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na kuapishwa na kuwa Waziri wa Ujenzi.
“Ninamshukuru Rais kwa kuendelea kuniamini, mimi pamoja na Naibu Waziri tunamuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kupambana na kudhibiti Rushwa hasa kwenye maeneo ya mikataba, manunuzi na usimamizi wa miradi, ili dhamira ya Rais na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi uende vyema,” amesema.
Aidha, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Katani Ahmed aliyetaka kujua lini Serikali itatenga fedha ya dharura kujenga kipande cha Barabara ya Nguja - Mkwiti - Tandahimba yenye maeneo korofi.
Bashungwa amewaagiza Mameneneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mikoa yote kufanya upembuzi yakinifu na kubaini maeneo yote korofi ya barabara na kuyawasilisha wizarani ili yaweze kupewa kipaumbele wakati wa kuandaa bajeti.
“Nitumie nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wa Tanroads mikoa yote kuangalia maeneo yote korofi na kufanya upembuzi yakinifu na kuyawasilisha Wizarani ili yapewe kipaumbele wakati wa kuandaa bajeti,” amesema Bashungwa.
Kadhalika, Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed alitaka kujua Je, ni lini ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi utaanza, ambayo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020 na ahadi ya Rais.
Wakati akijibu swali hilo, Bashungwa amesema ujenzi wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi yenye urefu wa kilometa 210 unatekelezwa kwa awamu ambapo ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mtwara – Mnivata (km 50) umekamilika kwa kutumia fedha za ndani.
Bashungwa amesema kuwa sehemu ya barabara ya Mnivata – Newala - Masasi (km 160) chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesainiwa tangu Juni 21, 2023 kwa sehemu za Mnivata – Mitesa (km 100) na Mitesa – Masasi (km 60) pamoja na ujenzi wa Daraja la Mwiti, kwa sasa Makandarasi wa sehemu zote mbili wapo katika hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi.