Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Basi la Shari Line laua tisa lajeruhi 18

Askari wa Usalama Barabarani akitazama basi la Kampuni ya Shari Line baada ya kutumbukia kwenye korongo katika kijiji cha Itamboleo, Kata ya Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema ajali hiyo ilitokea jana, Septemba 3, 2024 saa moja usiku katika kijiji cha Itamboleo, Kata ya Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya

Mbeya. Watu tisa wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Shari Line walilokuwa wakisafiria kutumbukia  kwenye korongo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 4, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema  ajali hiyo ilitokea jana, Septemba 3, 2024 saa moja usiku katika kijiji cha Itamboleo, Kata ya Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Amesema miongoni mwa majeruhi 18 ni dereva wa basi hilo, Alfredy Mwidunda (50), mkazi wa Ubaruku, Wilaya ya Mbarali ambaye amelazwa katika Hospitali ya Chimala Mission kwa matibabu zaidi akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Kamanda huyo amesema basi hilo lililokuwa linatokea Sumbawanga kuelekea Ubaruki na lilipofika eneo la Kijiji cha ya Mbarali kwenye kona kali dereva alishindwa kuimudu.

“Dereva wa basi hilo la Kampuni ya Shari Line alishindwa kuimudu kona ile akagonga gema na basi likatumbukia korongoni,” amesema kamanda huyo.

Muonekano wa basi la Kampuni ya Shari Line baada ya kutumbukia kwenye korongo katika kijiji cha Itamboleo, Kata ya Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Amesema bado miili ya marehemu haijatambuliwa na kati ya maiti hizo tisa wapo watoto wawili wa kike na mmoja wa kiume.

Kamanda Kuzaga amesema miili yote imehifadhiwa katika Hospitali ya Chimala Mission na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Kuzaga amesema kati ya majeruhi 18, kuna wanawake 13, wanaume watano na watoto watatu.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari alipofika kwenye eneo hilo lenye kona kali licha ya kuwekewa alama.

Hata hivyo, Kamanda Kuzaga ameongeza kuwa bado wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa chanzo cha ajali hiyo.