Bawacha wamjibu Ndugai sakata la kina Mdee

Bawacha wamjibu Ndugai sakata la kina Mdee

Muktasari:

  • Siku moja baada ya Spika Job Ndugai kueleza sababu kwa nini Halima Mdee na wenzake 18 bado ni wabunge, Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limesema kiongozi huyo wa Bunge amekosea na hoja alizozitoa bungeni kueleza uhalali wao hazina mashiko.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Spika Job Ndugai kueleza sababu kwa nini Halima Mdee na wenzake 18 bado ni wabunge, Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) limesema kiongozi huyo wa Bunge amekosea na hoja alizozitoa bungeni kueleza uhalali wao hazina mashiko.

Akizungumza leo Jumanne Mei 4, 2021 katika mkutano wa Bawacha kuhusu kujibu alichokizungumza Ndugai bungeni jana, mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Susan Kiwanga amemtaka Ndugai kutoa ufafanuzi kwa nini kuna kauli mbili zinazokinzana kuhusu wabunge hao waliofukuzwa uanachama Chadema Novemba 27, 2021.

Jana bungeni mjini Dodoma Ndugai alimvaa mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kwa maoni yake kuhusu sakata la wabunge hao waliotimuliwa baada ya kwenda kuapishwa kuchukua nafasi za viti maalumu bila ya idhini ya chama hicho.

Kitendo hicho kilichofanyika zaidi ya miezi mitano iliyopita kimeibuka shinikizo kutoka kwa Chadema na wadau wengine kwa Bunge kuhusu uhalali wao na Nape ni miongoni mwao ambaye hivi karibuni alikosoa  uhalali wao  katika mdahalo wa demokrasia ya vyama vingi ulioendeshwa kupitia mtandao wa Zoom, akisema uamuzi wa Chadema wa kuwafukuza wabunge hao uheshimiwe.

Katika maelezo yake ya jana Ndugai aliishukia Chadema na wengine wanaosema amevunja Katiba kwa kupokea wabunge wasiokuwa na chama, akisema taarifa kuhusu wabunge hao aliyoletewa na Chadema ni sawa na kipeperushi.

“Aprili 20 naibu spika alisema ofisi ya spika haikuwa na taarifa rasmi kufukuzwa uanachama wa wabunge 19, jana spika ameonyesha barua aliyoipokea, tunataka ajitokeze aeleze umma ni lini alipokea barua hiyo.”

“Spika Ndugai pia amezungumzia suala la viambatanisho kwenye barua hiyo kwa kuwa ni hoja isiyokuwa na mashiko na wala sio mamlaka yake kudai viambatanisho..., inakuwaje si sawa,” amesema.

Amesema Bawacha wanataka kufahamu wakati CCM  kinamwandikia barua ya kumfukuza na kumvua uanachama Sophia Simba au wakati Chama cha Wananchi (CUF)  kinamuandikia barua kuwavua uanachama waliokuwa wabunge wake, alikuwa wapi na kwa nini hakudai viambatanisho.

“Utaratibu wa kudai nakala ya kikao ni kwa Chadema au na vyama vingine? Chama kiliandika barua kumjulisha maamuzi ya kikao kilichofanywa na kamati kuu kwa mujibu wa katiba ya chama, hata hivyo badala ya kujibu barua hiyo ameibuka miezi mitano baadaye na kuzungumza bungeni ambapo sio njia rasmi ya mawasiliano.”

"Ndani ya Bunge hakuna kiongozi yoyote wa Chadema ambaye angepata nafasi ya kujibu hoja hizo, katika barua iliyoandikwa na katibu mkuu wa chama ameiita kipeperushi kitendo ambacho ni dharau...,  wanawake tunasema hatutakubali," amesema.

Huku akieleza kuwa baraza kuu la Chadema litaketi kusikiliza rufaa za kina Mdee kwa mujibu wa katiba ya Chadema amesema, “kukata rufaa hakutengui maamuzi ya awali mpaka hapo rufaa hiyo itakaposikilizwa na maamuzi kutolewa tofauti na awali, spika kutochukua hatua kwa kisingizio cha rufaa kupinga maamuzi ya awali inaonyesha namna gani ameamua kuingilia mambo ya ndani ya chama.”