Beatrice anayedaiwa kumuua mumewe apandishwa kizimbani
Beatrice Elias (36), mkazi wa Katanini anayetuhumiwa kumuua mumewe akiwa nyumbani kwa mzazi mwenzake.
Muktasari:
- Tukio la mauaji ya mfanyabiashara Evagro Msele lilitokea usiku wa kuamkia Mei 25, mwaka huu katika Kitongoji cha Pumuani A
Moshi. Beatrice Kwai (36), mkazi wa Katanini amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, mkoani Kilimanjaro, akikabiliwa na kosa la mauaji ya mume wake, Evagro Msele (43).
Tukio hilo la mauaji ya mfanyabiashara huyo maarufu mjini hapa, lilitokea usiku wa kuamkia Mei 25, mwaka huu, katika Kitongoji cha Pumuani A, baada ya mwanamke huyo kudaiwa kumvizia mumewe akiwa nyumbani kwa mzazi mwenzake kisha kumshambulia kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni kisu.
Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Msele, wakiwamo watoto wake, walifika mahakamani kushuhudia kinachoendelea leo Jumatatu, Juni 10, 2024.
Beatrice Kwai (36), anayetuhumiwa kumuua mumewe, akiwa amejifunika katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi leo Juni 10, 2024. Picha na Omben Daniel
Mwanamke huyo akiwa amevaa nikabu, aliletwa na gari binafsi na kuingia mahakamani kwa kupitia mlango wa nyuma.
Akisoma shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Herieth Mhenga, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Henry Daudi alidai kuwa Mei 25, 2024, mshitakiwa huyo alimuua Msele kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
"Mheshimiwa hakimu, mbele ya Mahakama hii tukufu, mshitakiwa yupo hapa kwa ajili ya kusomewa mashitaka ya makosa ya kesi hii mpya ya mauaji inayomkabili,” amedai Daudi.
Amedai kuwa, Mei 25, mwaka huu, Beatrice (36) akiwa eneo la Pumuani alitekeleza mauaji hayo kinyume cha sheria.
Baadhi ya ndugu wa Evagro Msele (43) wakiwa ndani ya viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi leo Juni 10, 2024. Picha na Janeth Joseph
Baada ya kusomewa shitaka hilo, Hakimu Herieth alimweleza mshitakiwa kuwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
"Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili mpaka hapo upelelezi upande wa mashitaka utakapokamilika, hivyo shauri hili litapelekwa Mahakama Kuu pindi upelelezi wa shauri hili dhidi yako litakapokamilika,” ameeleza Hakimu Herieth.
Hivyo, mwendesha mashitaka wa Serikali aliomba shauri hilo kupangiwa tarehe nyingine kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
"Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hili kuja kutajwa," amesema Daudi.
Mshitakiwa amerudishwa rumande mpaka kesi hiyo itakapotajwa Juni 25, mwaka huu.