Bei elekezi za vifurushi kuanza kutumika leo

Bei elekezi za vifurushi kuanza kutumika leo

Muktasari:

  • Leo Watanzania wameanza kupata uzoefu mpya katika huduma za simu kutokana na kuanza kutumika kwa kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalumu.

Dar es Salaam. Leo Watanzania wameanza kupata uzoefu mpya katika huduma za simu kutokana na kuanza kutumika kwa kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalumu.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba aliahidi kuwa utekelezaji wa kanuni za kukabiliana na malalamiko juu ya huduma ya vifurushi zinazotolewa na kampuni mbalimbali za simu nchini utaanza Aprili 2, 2021.

Kanuni hizo ziliandaliwa kufuatia maoni 3,278 yaliyotolewa na wananchi kuhusu vifurushi hivyo. Baadhi ya mitandao ya simu jana iliwataarifu watumiaji wake juu ya hayo mabadiliko yanayoanza leo.

Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji TCRA, Dk Philip Filikunjombe alisema baadhi ya changamoto walizokuwa wakikutana nazo watumiaji wa huduma za simu ni pamoja na gharama za vifurushi kuwa juu na vifurushi vya data kubadilika mara kwa mara.

Dk Filikunjombe alisema vilevile watumiaji walilalamikia kutumiwa ujumbe mfupi wa simu bila ridhaa yao, watumiaji kupoteza GB katika bando pale muda wa bando unapokwisha ilhali bado GB hazijaisha, utitiri wa bando zinazotolewa na watoa huduma pamoja na kwisha haraka.


Nini maoni yako bei mpya za vifurushi?