Bei mpya za vifurushi mjadala mitandaoni

Bei elekezi za vifurushi kuanza kutumika leo

Muktasari:

  • Mapema leo Ijumaa Aprili 2, 2021  mjadala umekuwa mkubwa miongoni mwa watumiaji simu za mkononi baada ya mambo kuwa kinyume na matarajio yao licha ya kuanza kutumika kwa kanuni mpya za huduma.

Dar es Salaam. Mapema leo Ijumaa Aprili 2, 2021  mjadala umekuwa mkubwa miongoni mwa watumiaji simu za mkononi baada ya mambo kuwa kinyume na matarajio yao licha ya kuanza kutumika kwa kanuni mpya za huduma.

Kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) zimeanza kutumika leo matumaini ya wengi ilikuwa ni bei za vifurushi kupungua lakini imekuwa tofauti.

Bei mpya za vifurushi mjadala mitandaoni

Mwanzoni mwa Machi, 2021 mkurugenzi mMkuu wa TCRA, James Kilaba aliahidi utekelezaji wa kanuni hizo za kukabiliana na malalamiko juu ya  huduma ya vifurushi yaliyotokana na maoni 3, 278 yaliyotolewa na wananchi.

Baadhi ya changamoto ambazo watumiaji wa huduma za simu walikuwa wakikutana nazo na kuzilalamikia ni pamoja na gharama za vifurushi kuwa juu na vifurushi vya data kubadilika mara kwa mara.

Jana mitandao ya simu iliwataarifu watumiaji wake juu ya mabadiliko hayo yanayoanza leo lakini jambo ambalo limewaibua wengi hususani katika mitandao ya kijamii ni kuminywa kwa vifurushi hivyo kuliko hata ilivyokuwa awali wakati wanatoa malalamiko hayo.

Bei elekezi za vifurushi kuanza kutumika leo

Katika makundi ya mtandao wa kijamii wa Whatsapp na mitandao  mingine ya kijamii inayokutanisha watu kama Twitter, Instagram na Facebook mjadala ni vifurushi ambavyo vimebadilika katika mitandao yote ya huduma za simu wengi wanaomba walau hali irudi kama ilivyokuwa.

Mitandao mbali ya simu kama ilivyo ada katika sikukuu mbalimbali ilituma salamu zao za sikukuu kupitia kurusa zao za mitandao ya kijamii lakini maoni ya wananchi wengi si kupokea salamu hizo bali ilikuwa ni kulalamikia mabadiliko yaliyofanywa katika vifurushi.

Mtumiaji mmoja wa mtandao wa Twitter anayetumia jina la Dady aliandika katika mtandao huo,“ kutokana na bei za vifurushi zilizopo sasa watu wataanza kutumia barua katika mawasiliano kama ilivyokuwa zamani”.

Malopa yeye alisema “Yaani tarehe 2 mwezi wa 4 mabadiliko ya vifurushi ndio imekuwa na maumivu zaidi kiasi hiki. Bora kabla ya tarehe hii vilikuwa na unafuu. Tunajuta kuingia uchumi wa kati, kula kwenyewe tabu na mnazidi kupandisha tu gharama za vifurushi, daah! Mnatutesa sana jamani!”

Naye Eddy aliandika Twitter kuwa, “mnatuambia tujiunge vifurushi vya gharama tunazo zimudu ilhali hizo bando tulizokuwa tunajiunga mmezipunguza ujazo now 500 unapata Mb's chache tofauti na mwanzo mnategemea tutatoboa kweli? Kaeni chini na Serikali mkubaliane wawashushie kodi hivi mnatuumiza watumiaji wa mwisho.”