Bei ya petroli, dizeli yashuka Zanzibar

Meneja Kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Hassan Haji akitangaza mabadiliko ya bei ya mafuta mjini Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

What you need to know:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza bei mpya za mafuta huku inyosha kushuka kwa bidhaa hiyo ambapo wakati dizeli imeshuka kwa asilimia tatu, petroli ikishuka kwa asilimia mbili.

Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza bei mpya za mafuta huku inyosha kushuka kwa bidhaa hiyo ambapo wakati dizeli imeshuka kwa asilimia tatu, petroli ikishuka kwa asilimia mbili.

Wakati bei hizo zikitarajiwa kuanza kutumika kesho Julai 9, 2023, lita moja ya mafuta ya petroli itauzwa kwa Sh2, 730 kutoka Sh2, 780 za awali huku dizeli Sh2, 800 kutoka Sh2, 900.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Juni 8, 2023 ofisini kwake Maisara, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Hassan Haji, amesema pia mafuta ya ndege yatauzwa kwa Sh2, 345 kutoka Sh2500 huku mafuta ya taa yakibaki katika bei yake ya awali Sh2, 921.

“Zura inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani kwa mwezi uliopita, ili kupata kianzio cha kufanyika mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi huu,” amesema.

Amesema jingine ni kuangalia gharama za uingizaji mafuta katika bandari ya Dar es salam, kuangalia thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola za kimarekani, gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi za serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Amesema mabadiliko hayo yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika Soko la Dunia, thamani ya dola ya Marekani pamoja na Serikali kuendelea kupunguza makali ya bei ya mafuta hasa kwa mafuta ya dizeli kutokana na bidhaa hiyo kuwa tegemezi zaidi katika harakati za kiuchumi kwa Zanzibar.

Mmoja wa wakazi wa mjini Unguja Abubakar Haji amesema licha ya kupungua kiwango hicho katika mafuta bado yapo juu ikilinganisha na hali halisi ya maisha ya wananchi kwani mafuta ndio msingi wa kila kitu.

Kwa upande mwingine, taarifa kutoka Serikalini zinaonyesha kuwa baada ya kuzinduliwa kwa Bohari Mwangapwani, yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 21 za mafuta, hivyo Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuhifadhi mafuta yake yenyewe tofauti na ilivyo sasas kuhjifadhiwa katika bandari ya Tanga.

Bohari nyingine ni zile zilipo Mtoni zenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 16.