Bernard Membe alitimiza nguzo zote sita za ujasiri

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaitaifa, Bernad Membe enzi za uhai wake.

Dar es Salaam. Maneno ya Kiingereza yenye kubeba tafsiri ya ujasiri ni mengi. Hapa nitatumia mawili, “valorous” na “plucky,” kueleza wasifu wa Bernard Kamillius Membe, mwanasiasa, mwanadiplomasia na kachero aliyebobea.

‘Valorous,’ mwenye kuonesha ujasiri hata mbele ya hatari.

‘Plucky,’ asiyeyumba katikati ya nyakati ngumu. Tafsiri zote hizo zinamgusa Membe, mbunge wa Mtama kwa miaka 15, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka nane.

Miaka mitano ya utawala wa Rais wa tano, John Magufuli, ulimdhihirisha zaidi Membe.

Si mwoga, hapendi kushindwa, anaweza kupambana mpaka pumzi ya mwisho. Kunyanyua mikono na kusalimu amri, hiyo kwake ni mwiko.

Fanya marejeo; wakati wa Magufuli kulitokea fukuto la kisiasa ndani ya CCM. Hesabu mmoja baada ya mwingine waliotuhumiwa kumhujumu Magufuli, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM.

Utaona kuwa wote, hata wale walioonesha mwanzoni ni wagumu, hatimaye walisalimu amri, isipokuwa Membe.

Kituo kimoja baada ya kingine, Membe alibaki yuleyule. Na njia alizozichagua katika mgogoro wa kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), uliohusisha wengi, tena watu wazito, Membe alikuwa na namna ya peke yake ya kuushughulikia.

Alikwenda mahakamani kumshtaki Cyprian Musiba, kada wa CCM, aliyejitambulisha kuwa ni mwanaharakati mtetezi wa Magufuli. Ni baada ya Musiba kumtaja Membe kuwa anamhujumu Magufuli.

Wengi walitajwa na Musiba, ikiwamo kutamkwa isivyofaa. Wapo waliokaa kimya, walikuwepo waliolaumu na kutishia kuchukua hatua, lakini hawakufanya kitu. Membe, Wakili Fatma Karume na Waziri wa Ardhi wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka, walishinda kesi na Mahakama iliamuru walipwe fidia.

Agosti 11, 2021, Mahakama Kuu Zanzibar ilimhukumu Musiba kumlipa Fatma, Sh7.5 bilioni kwa kumdhalilisha. Agosti 13, 2021, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilimwamuru Musiba kumlipa Profesa Tibaijuka Sh80 milioni kwa kumchafua.

Oktoba 28, 2021, Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, ilimwamuru Musiba kumlipa Membe, Sh6 bilioni.

Fatma na Tibaijuka wamekuwa wakijivuta kukazia hukumu, lakini Membe alishatangulia mbele na tayari wajibu wa kudai upo kwa dalali wa Mahakama, Kampuni ya Yono.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Uamsho Tanzania, Bandekila Mwamakula alimwandikia barua Membe, kumwombea msamaha Musiba. Hata hivyo, Membe alijibu kuwa asingemsamehe abadan!

Bora kutoeleweka lakini sharti usimamie kile unachoona ni sahihi kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi utu wako. Hicho ndicho Membe alikisimamia. Na ndio kinaitwa “ujasiri wa kiroho” – “spiritual courage.”

Huyo ndiye Membe. Watu aina yake ndio wale husemwa waliumbwa na “moyo wa simba” – “lionhearted.”

Anapotaka lake lazima alipiganie. Akianzisha vita sharti ifike mwisho. Kuonewa kwake mwiko. Kumvunjia heshima usijaribu, mtamalizana.


Alichelewa kujulikana

Msimamo wa Membe wa kukataa kuburuzwa kipindi cha uongozi wa Magufuli, ulifanya watu wengi wamfahamu Membe. Alijitosheleza kwa ujasiri wa kijamii (social courage) na ujasiri wa kimwili (physical courage).

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, alitangaza kusudio lake la kukutana na Membe ili amhoji kwa nini anatajwa kumhujumu Magufuli.

Haukupita muda, Membe alijibu alikuwa tayari wakati wowote kuitikia wito. Alipoona anachelewa kuitwa, alihoji: “Nasubiri wito, mbona siitwi?”

Kamati ya Maadili ya CCM iliwaita Membe na makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusuf Mamba. Membe alikuwa wa kwanza kujibu kuwa angeitikia wito.

Membe alihudhuria kikao na alipotoka, alizungumza kwa kujiamini: “Tulikuwa na mkutano wa saa tano, wa mijadala mizuri, mikubwa ya kitaifa, inayohusu Chama cha Mapinduzi na nchi yetu. Nina furaha kubwa ajabu. Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo ambayo chama changu kilitaka kuyajua.”

Kitendo cha Membe kuitikia wito wa mamlaka za CCM, kwenda kuzungumza bila hofu katikati ya vitisho vingi vilivyokuwepo, hicho ndicho huitwa ujasiri wa kisomi (intellectual courage).

Misimamo ya Membe ilifanya watu wajiulize nini kilimbadilisha. Hapana, nyakati zilimdhihirisha. Hakuna wakati wowote Membe hakuwa Membe.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, aliyekuwa Waziri Mkuu wa UK, David Cameron, alipotoa sharti kuwa kila nchi inayoendelea na ambayo inapokea misaada kutoka kwao, lazima itunge sheria ya kuruhusu ndoa za jinsia moja, Membe alijibu:

“Tupo tayari kwa lolote, hatuwezi kuvunja utaifa na utamaduni wetu kwa nchi yoyote tajiri inayotoa masharti ya kipuuzi ili tushibe matumbo yetu. Kama wanadhani misaada ndio silaha yao wakae nayo.”

Jibu hilo la Membe ndiyo mantiki ya “ujasiri wa kimaadili” – “moral courage.”

Kusimamia kilicho sahihi kwa gharama yoyote. Balozi wa UK Tanzania, alimjibu Membe kuwa sharti alilotoa Cameron halikuihusu Tanzania.

Chokochoko za kikundi cha waasi M23, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuitisha Tanzania, ziliifanya Afrika itambue kuwa Tanzania ilikuwa na Membe, Waziri wa Mambo ya Nje, mwenye misimamo mikali na ambaye msamiati wa woga haupo kichwani kwake. Membe akawaahidi M23 kichapo. M23 walikiona cha moto.

Ni Membe aliyeifanya Tanzania iwe nchi pekee Afrika iliyotoa msimamo wa kulaani mataifa makubwa ya Marekani na washirika wake, walipoivamia Libya mwaka 2011 na kumuua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.

Membe alisema, dhamira haikuwa kumwondoa madarakani Gaddafi, bali kumuua. Ni ‘moral courage!’

Mwaka 2008, Membe alikuwa kiongozi pekee wa Kiafrika mwenye kuhusika na mashauri ya kigeni, aliyeisema Zimbabwe, iliyokuwa ikiongozwa na Robert Mugabe, kwamba ilikuwa haioneshi kwenda kwenye uchaguzi huru na haki. Na baada ya uchaguzi, Membe alisema Zimbabwe haikuwa na jinsi zaidi ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kauli za Membe zilikichukiza chama tawala Zimbabwe (ZanuPF). Membe hakupindisha kauli. Yupo mwanachama mwandamizi wa ZanuPF, anayeitwa Joram Jumbo, alitoa maneno makali mno kumshambulia Membe.

Mwisho, Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa Zimbabwe. Mugabe akawa Rais, mpinzani wake, Morgan Tsvangirai, akawa Waziri Mkuu.