Biashara bunifu zinavyofungua fursa mpya kwa vijana

Muktasari:
- Kwa kusaidiwa kupitia programu kama Vodacom Digital Accelerator, biashara hizi hupata si tu maarifa ya kitaalamu na mitaji, bali pia jukwaa la kuonekana na kuunganishwa na wawekezaji na wadau muhimu.
Dar es Salaam. Katika kile kinachoonekana kuwa ni hatua muhimu ya kuinua vipaji vya ubunifu na ujasiriamali nchini, Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Huawei Tanzania, wamezindua rasmi msimu wa nne wa programu ya Vodacom Digital Accelerator (VDA), tukio lililofanyika jijini Dar es Salaam mnamo Mei 9, 2025.
Kwa mwaka huu, jumla ya biashara bunifu 15 zimefanikiwa kuingia kwenye programu hiyo, ambapo zitashiriki katika mafunzo ya siku tano ya Design Sprint yanayoendeshwa na wataalamu wa kimataifa kutoka Marekani kupitia programu ya MassChallenge.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Zuweina Farah, amesema: “Tunaamini VDA ni jukwaa sahihi la kukuza kizazi kijacho cha wavumbuzi wa Kitanzania. Kwa kushirikiana na wataalamu wa kimataifa, tunawaletea vijana uzoefu wa kimataifa na nyenzo muhimu kwa ajili ya kukuza biashara zao.”
Katika mafunzo hayo, biashara hizo zitawezeshwa kuboresha bidhaa zao, kuimarisha nafasi yao sokoni, pamoja na maandalizi ya kuvutia wawekezaji. Baada ya hatua hiyo ya awali, biashara 10 kati ya 15 zitachaguliwa kuingia kwenye hatua ya pili ya maendeleo ya kina kwa kipindi cha miezi mitatu.
Katika hatua hiyo, zitapata msaada wa kitaalamu, kuunganishwa na masoko ya ndani na nje, pamoja na fursa ya kusafiri nchini China mwezi Juni ambako watakutana na makampuni makubwa ya teknolojia na wawekezaji binafsi.
Kwa mujibu wa waandaaji, msimu huu pia utahusisha uwekezaji wa moja kwa moja wa fedha taslimu kwa biashara tatu bora, ili kusaidia kukuza ubunifu wao na kuwaongezea ushindani katika soko la ndani na kimataifa.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, Vodacom Digital Accelerator imewawezesha zaidi ya biashara 75 chipukizi nchini kwa kuwapatia nyenzo, mtaji na mitandao ya biashara. Msimu huu mpya unalenga zaidi ujumuishwaji wa kidijitali, uhifadhi wa baiyoanuai, na ujasiriamali kwa vijana.
Kwa biashara nyingi changa nchini, VDA inazidi kuwa mwanga wa matumaini na daraja la mafanikio katika dunia ya teknolojia.
Biashara bunifu ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika zama za sasa. Kupitia ubunifu, biashara hizi huleta suluhisho jipya kwa changamoto za kila siku, huongeza tija, na huibua ajira kwa vijana. Zaidi ya hapo, bunifu huwezesha ushindani wa haki sokoni kwa kutumia teknolojia na maarifa ya kisasa, jambo linalowasaidia wajasiriamali wa ndani kuvuka mipaka ya kibiashara na kufikia masoko ya kimataifa.