Biashara ya kutisha Dar, Wajanja wanavyojinufaisha na walemavu ombaomba (3)
Muktasari:
Jana tuliishia sehemu ambayo mwandishi wetu ameelezwa jinsi wajanja wanavyojinufaisha na walemavu wanaoombaomba na akapewa namba ya simu ya mmoja wa watu wanaojishughulisha na biashara ya kutumia walemavu kuombaomba mitaani. Leo, mwandishi wetu anasimulia jinsi walemavu wanavyoishi kwenye nyumba waliyopangishiwa eneo la Manzese. Endelea...
Dar es Salaam. Lakini sikutaka kuharakisha kwenda kwa kijana huyo, badala yake nikaamua kwanza kumfuatilia Shadrack.
Siku niliyoenda Gerezani nilimkuta mtoto anayesukumwa na Shadrack akiwa peke yake na nilipomsogelea alisema tena “dada” kama alivyofanya siku ya kwanza.
Nilipomsogelea akanionyesha ishara kuashiria kuwa kuna kitu chini ya kiti chake.
Bila shaka alihitaji msaada wa maji ya kunywa kwa kuwa chini ya kiti kulikuwa na chupa ndogo ya maji.
Nikaiokota, kuifungua kisha kunywesha maji na baadaye nikamuuliza alipo mjomba wake, lakini akajibu kwa kusema tena “dada” huku akitabasamu.
Muda mfupi baadaye akaja kijana na kusimama pembeni yangu akijifanya kuongea na simu. Nikasogea pembeni, lakini akaniufuata kijana mwingine na kunidadisi.
“Dada, eti huyo mtoto ana shida gani,” aliniuliza kijana huyo na nikamjibu kuwa alikuwa anahitaji maji ya kunywa na nimeshampa.
“Ooh! Ila hawa watoto wana shida sana,” anasema huku akiondoka.
Ninatoka eneo hilo nakwenda kukaa ndani ya kituo cha daladala nikisubiri muda ambao Shadrack anatoka ili nimfuatilie na kujua anapotoka hapo huwa anaelekea wapi?
Baada ya kumsubiri kwenye kituo cha mwendokasi hadi saa 12:00 jioni bila kumuona, naamua kumsogelea ombaomba mmoja na dakika 12 baadaye anakuja kijana mmoja aliyekuwa akimsukuma mtoto mwenye umri unaokaribia miaka minane. Huyu ni mlemavu wa miguu na mikono na pia ni bubu.
Baadaye kijana huyo anamwacha mlemavu wake na kwenda kwa yule wa Shadrack. Anamuweka vizuri na baada ya dakika takriban tatu, akaja kijana mwingine na kumchukua ombaomba mwingine ambaye alikuwa amelala chini.
Baadaye niligundua anaitwa Pili Iyobhe. Huyu nilipeleleza habari zake hadi nikapata taarifa za kutosha kuwa anatokea mkoani Shinyanga, na hivyo ikawa rahisi kumfuatilia hadi nyumbani kwa wazazi wake.
Mtoto huyo wa kike ana tatizo la kichwa kikubwa na muda mwingi anakuwa amefumba macho. Tofauti na wenzake wenye baiskeli, alikuwa amelala chini.
Lakini kijana aliyemfuata, anambeba na kumuweka kwenye baiskeli kisha kwenda kwa kijana aliyekuwa akimrekebisha mtoto anayesukumwa na Shadrack.
Baada ya muda mfupi, vijana wapatao saba wanakusanyika eneo hilo na kujadili jambo fulani, na baadaye kusambaa kila mtu njia yake na dakika 10 baadaye kila mmoja anamchukua mlemavu wake na kwenda naye kupanda basi la mwendokasi.
Kutokana na kuwa na walemavu, walipitiliza kukata tiketi badala ya kupanga foleni kama abiria wengine. Wakati naendelea kushuhudia hayo, akatokea Shadrack mnamo saa 1:00 usiku akiwa ameshamchukua yule mlemavu aliyekuwa amemuacha.
Wakati anakata tiketi, nikamuuliza anakoelekea na kunijibu kuwa anapanda basi la Kimara, nami nikapanda basi hilo lakini nikamuona anashukia kituo cha Bakhresa eneo la Manzese. Nami nikashuka na kuanza kumfuatilia kuelekea Tandale.
Akaingia kwenye nyumba mmoja ya kulala wageni, ambayo jina tunalihifadhi na juu ya geti kuna namba za simu (ambazo pia tunazihifadhi kwa sababu za kimaadili).
Nyumba hiyo imezungukwa na nyumba nne na nje ya geti kuna mama anapika sambusa.
Baada ya kununua sambusa mbili naanza kumhoji kuhusu nyumba hiyo na wateja wake.
“Hii ni gesti mwanangu na nafasi zipo. Kama unataka wewe ingia tu ndani utawakuta wahusika,” anasema.
Nami naingia ndani ambako nakuta baiskeli nne za walemavu zikiwa zimesimamishwa kwenye mlango wa kuingilia vyumbani na nyingine tatu zikiwa nje, pia alikuwapo Shadrack aliyekuwa anaongea na simu huku akiwa ameshikilia baiskeli yake iliyokuwa na mtoto mlemavu.
Ndani ya nyumba kulikuwa na sauti ambazo baadaye nilibaini zilikuwa za watu waliokuwa wakizungumza Kisukuma.
Baadaye akatoka kijana mrefu na nilipomuuliza kuhusu vyumba, alinijubu kuwa mhusika anaitwa Jose na akaenda kumuita.
“Jose amekwenda wapi?” anawauliza wenzake kwa kutumia lugha ya Kisukuma na wanamjibu kuwa ametoka kidogo.
Nikiwa nasubiri, namsikia Shadrack akiendelea kuongea na simu akisema: “Nakwambia jamani, uje unisalimie tu. Kwani ukija kunisalimia ni vibaya? kwa nini hivyo? Uje bwana unisalimie nimesharudi.”
Nyumba hiyo ina korido ndefu yenye vyumba vidogo kila upande. Chumba cha kwanza hakikuwa na mtu aliyepanga ila vyumba vilivyobaki vilikuwa na watu ndani na katika korido kuliegeshwa baiskeli mbili za walemavu.
Baada ya kushuhudia hayo, nilienda nje na kukaa eneo ambalo vijana walikuwa wakiuza ndizi, mbali kidogo na nyumba hiyo ya wageni.
Nikiwa nimekaa eneo hilo, alipita mlemavu mwingine akiwa anasukumwa kwenye baiskeli na kijana mdogo anayekadiliwa kuwa na miaka 16.
“Samahani kaka naomba kuuliza mara nyingi nikiwa maeneo haya huwa ninaona walemavu wengi wanapita hapa, wanakwenda wapi?” niliuliza vijana niliokaa nao.
“Pole dada hujui wanapokwenda? Mradi wa mtu huo,” alijibu mmoja wao huku wengine wakicheka.
Alisema hiyo ni biashara mpya imeingia mjini na kuna watu wanaowachukua walemavu kutoka vijijini na kuwaleta mjini kufanya kazi ya kuombaomba.
“Dili hilo dada,” alisema kijana mwingine.
“Tena mmoja wa wanaofanya biashara hiyo alikuwa maeneo hayahaya. Sijui kaenda wapi? Hii ndiyo biashara inayomuweka mjini.”
Siku tatu ndani ya gesti
Taarifa za biashara hiyo zilinifanya niamue kupanga ndani ya nyumba hiyo, nikijifanya mmoja wa wa wageni, kwa lengo la kujua walemavu hao wanaishije ndani ya nyumba hiyo, wametokea wapi, nani anawaleta na wanafanyaje shughuli hiyo.
Siku nilipokuja kuchukua chumba, nilimkuta mwanamke mjamzito akifua nguo na baada ya kumuuliza mhusika, alinipa namba za simu za nyumba hiyo.
Baada ya kumpigia, kijana aliyepokea alijitambulisha kwa jina la Jose na kuniomba nimsubiri na baada ya takriban dakika 10 aliingia.
“Chumba kimebaki kimoja,” ananiambia na nikamuomba nikakione.
Ni chumba kidogo chenye kitanda cha ukubwa wa futi tatu kilichotandikwa shuka la maua ya rangi tofauti zilizofubaa.
Ndani ya chumba kulikuwa na feni na kiti kilichochakaa cha plastiki, taulo na choo kichafu. Kitanda hakikuwa na neti wala shuka la kujifunika. Kila kona ya chumba imechorwa alama ya msalaba wa rangi nyeusi.
Kuna ndoo moja ya lita 10 kwa ajili ya maji na choo kilikuwa kama kimeziba.
“Chumba ni Sh7,000,” alisema baada ya kumuuliza na baada ya kumuomba apunguze, alisema kama ningekuwa nakaa zaidi ya mwezi angenifanyia Sh6,000.
Nikamlipa Sh21,000 kwa ajili ya malipo ya siku tatu na nikajisajili kwenye kitabu cha wageni. Baadaye, nikatoka kuchungulia vyumba vingine vilivyokuwa vimeachwa wazi na inaonekana vyote vimefanana.
Katika kuulizauliza, niliambiwa alama hiyo ya msalaba ni kinga dhidi ya watu wanaofanya biashara haramu ya walemavu kwa imani za kishirikina.
Tofauti na sehemu nyingine, vyumba vitatu vilikuwa na vyombo na majiko ya kupikia, kama vile vyumba vya makazi na si vyumba vya kulala wageni.
Nikiwa nimekaa nje baada ya kumaliza uchunguzi wangu, namshuhudia mlemavu mmoja akirejea mnamo saa 1:00. Huyu ni mlemavu wa miguu hivyo anatembea kwa kutumia mikono. Lakini katika kazi, anatumia baiskeli akisukumwa na kijana.
Baadaye wakaanza kumiminika mmoja baada ya mwingine. Kila anayefika, humwaga kitandani fedha alizopata na kuzihesabu na wakati huo, hufunga mlango kuzuia watu kuingia.
Saa 4:00 usiku anaingia mwanamke mnene kuwaletea chakula; wali na maharage. Muda huo, walemavu hao hutengewa chakula jirani na choo.
Wanaowasukuma hutoka nje kuchukua chakula kilichowekwa kwenye mifuko ya rangi nyeusi na kuingia nacho vyumbani kwa ajili ya kula.
Aina ya walemavu
Ndani ya nyumba hii ya wageni kuna walemavu 13 na kati ya hao watatu ni wa kike. Wawili wana ulemavu wa kichwa kikubwa, pia yuko mlemavu ambaye amepooza mikono na miguu, ambaye jina lake ni Ndebhile ambaye kwa kipindi nilichokuwapo hapo amekuwa akitengewa chakula peke yake jirani na mfereji wa maji machafu.
Pia, wapo ambao miguu yao imepinda na wanatembea kwa kutumia mikono, mmojawao akiwa ni Ndebhile.
Ni miongoni mwa walemavu wakorofi na wagomvi, muda wote anakuwa na hasira na anapotembea hataki mtu akatize mbele yake kwa kuwa hutembea kwa kasi.
Mlemavu huyu anaongea vizuri kuliko walemavu wengine ambao baadhi hawawezi kuongea na wapo ambao wanaongea kwa tabu.
Kati ya hao 13, ni wawili tu ambao wana akili timamu na wanaojitambua, yaani Pili na Iyobhe au Dorcas ambaye nilimkuta akiwa amebebwa eneo la Gerezani na mama Juma.
Mama Juma ana mtoto mmoja wa kiume na Dorcas hana mtoto. Walemavu hawa ndiyo wenye uwezo hata wa kuzungumza na kueleza jambo lolote wanalolijua. Walemavu wengine hawajitambui na wala hawajui chochote.
Walio wengi ni wadogo wenye umri kati ya miaka saba na 15. Vijana wanaowasukuma ni wenye nguvu na walioshiba.
Mara nyingi vijana hawa wanaporudi katika nyumba hii huonekana wakizungumza na simu kwa kilugha.
Itaendelea kesho