Biden aapishwa akiahidi demokrasia

Biden aapishwa akiahidi demokrasia

Muktasari:

  • Sasa ni rasmi Joe Biden ni Rais wa 46 Marekani baada ya kula kiapo leo Jumatano Januari 20, 2021 akipokea kijiti kutoka kwa Donald Trump.

Marekani. Sasa ni rasmi Joe Biden ni Rais wa 46 Marekani baada ya kula kiapo leo Jumatano Januari 20, 2021 akipokea kijiti kutoka kwa Donald Trump.

Biden amekula kiapo mbele ya jaji wa Mahakama Kuu,  John Roberts na mbele ya wafuasi wake waliofurika katika Ikulu ya White House Marekani.

Baada ya kula kiapo Biden amelihutubia Taifa hilo kwa mara ya kwanza huku akiwashukuru watangulizi wake akiwemo mwasisi wa Taifa hilo, George Washington.

Marais wastaafu Bill  Clinton, George Bush na Barack Obama wamehudhuria sherehe hiyo.

''Hii ni siku ya kidemokrasia. Ninawashukuru watangulizi wangu wa vyama vyote walio hapa  leo,'' amesema.

Amebainisha kuwa atakuwa kiongozi wa Wamarekani wote na kuahidi kuwa kwa pamoja watalishinda gonjwa la Covid 19.

Kuhusu demokrasia amesema itaendelea kuheshimiwa na kuwepo, akiwataka wananchi kuheshimiana na kupendana.

Biden amesema alizungumza kwa simu na Rais mstaafu wa nchi hiyo Jimmy Carter (96) na kumpongeza kwa utumishi wake.

Hata hivyo, katika hafla hiyo Trump hakuhudhuria aliondoka Ikulu ya Marekani akiwa na mkewe, Melania na kuelekea katika kambi ya jeshi ya Maryland alikofanyiwa sherehe za kumuaga.

Baada ya shughuli hiyo Trump na mkewe wamesafiri kwa ndege ya Air Force One kwenda Florida ambako atakuwa akiishi katika makazi yake ya kifahari.

Badala ya Trump, makamu wake, Mike Pence alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Biden na hakuenda kumuaga Trump.