Biteko aeleza majukumu ya Tanzania uenyekiti ADPA

Muktasari:

  • Tanzania itapokea uenyekiti wa jumuiya ya vchi zinazozalisha madini ya Almasi barani Afrika (ADPA) wakati wa mkutano wa mawaziri wa watalaam wa madini kutoka nchi 12 wanachama utakaoanza leo Jumatano Aprili 7, 2021.

Dodoma. Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko amesema Tanzania ikiwa mwenyekiti wa jumuiya ya nchi zinazozalisha madini ya Almasi barani Afrika (ADPA), itajitahidi kuboresha mfumo wa jumuiya hiyo kuwa na manufaa kwa nchi wanachama kama ilivyokusudiwa.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 7,  2021, Biteko amesema Tanzania itapokea uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka Namibia ambayo imemaliza kipindi cha mwaka mmoja.

Amesema mkutano huo wa siku mbili utakaoanza leo utahusisha mawaziri na wataalam kutoka nchi 12 wanachama wa ADPA na utafanyika kwa njia ya mtandao.

“Mkutano wa mawaziri utatanguliwa na wataalam unaotarajiwa kufanyika leo na utajadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya ADPA  na mkutano wa Machi 8 wa mawaziri utahusika kutoa maamuzi ya masuala hayo,” amesema.

Amesema pamoja na majadiliano hayo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na nchi wanachama kuhusu  usimamizi wa sekta ya madini na kuimarisha utendaji katika wizara ambayo tunaisimamia.

Amesema katika kipindi cha uenyekiti watajitahidi kuhakikisha wanaboresha mifumo ya jumuiya ya ADPA ili iweze kuwa na manufaa kwa nchi wanachama kama ilivyokusudiwa.