Biteko: Mfanyeni kila anayekuja ofini kwenu aondoke na furaha
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka waandishi na waendesha ofisi (makatibu mahsusi) kuacha kauli za kuvunja moyo wananchi wanapofika kwenye ofisi zao kutatuliwa shida na changamoto wanazopitia.
Mwanza. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka waandishi na waendesha ofisi (makatibu mahsusi) kuacha kauli za kuvunja moyo wananchi wanapofika kwenye ofisi zao kutatuliwa shida na changamoto wanazopitia.
Akifungua mkutano mkuu wa 11 wa kitaaluma wa Chama cha Waandishi na Waendesha ofisi tanzania (Tapsea), jijini Mwanza leo Alhamisi Mei 23, 2023, Dk Biteko amewataka kurekebishana, wakibaini miongoni mwao kuna mwenye tabia na kauli mbaya za kuvunja moyo watu wenye shida ya kuonana na mabosi wao.
“Watanzania wengi watakuja kwenu kwa ngazi zenu wakiwa wanataka huduma miongoni mwenu, wanataka huduma nyingine kutoka kwa wakubwa wenu, lakini kabla ya kuwafikia wakubwa wenu watakutana na nyinyi, nyinyi muwe kielelezo cha kuwaonyesha nia ya kuwahudumia Watanzania… mfanyeni kila mmoja anayekuja ofisini kwenu atoke akiwa na furaha na kuamini kuwa kodi anayolipa inamlipa yeye mwenyewe kwa kupata huduma iliyo bora,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko amesema Serikali imeendelea kuboresha kazi ya kada hiyo kwa kuuisha muundo na kuleta maendeleo kwa kupanua wigo wa kujiendeleza kielimu na kupanda madaraja miongoni mwao, huku akiwataka kujiendeleza kitaaluma kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
“Baada ya maboresho haya sasa mtumishi huyu anaweza kuongezewa wigo wa elimu kutoka diploma hadi shahada ya uzamili, ambayo itamuwezesha kutoka daraja ‘G’ la mshahara hadi kufika ukomo wa daraja H la mshahara,” amesema.
Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Serikali imeendeleza jitihada za kuondoa kero na changamoto za watumishi, ikiwa ni pamoja na ya uhaba wa watumishi wa kada hiyo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 ilitangaza nafasi 414 mpya za ajira na ulipofika mwaka wa fedha 2023/24 iliidhinisha nafasi 722 mpya kwa kada hiyo.
“Kwa kutambua mchango mkubwa uliotolewa na kada hii katika ustawi wa umma, jumla ya waandishi waendesha ofisi 864 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2022/23 wameshapandishwa vyeo na kuidhinishiwa mishahara ya vyeo vipya Juni, 2023,”amesema.
Amesema Serikali pia imeidhinisha upandishaji vyeo vya watumishi 628 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24, akidai itaendelea kupandisha vyeo vya watumishi wengine kulingana na upatikanaji wa fedha.
Amesema mwaka 2022/23 Serikali imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara zaidi ya Sh236.6 milioni kwa watumishi wa kada hiyo huku mwaka 2023/24 ikiwalipa zaidi ya Sh249.1 kwa watumishi 211.
Awali, Mwenyekiti wa TAPSEA, Zuhura Maganga amesema mkutano huo umeudhuriwa na washiriki 5, 000 kutoka serikalini na sekta binafsi ambao pia wamefundwa mambo mbalimbali, ikiwemo mfumo wa usimamizi wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na taasisi, maadili katika utumishi wa umma, utunzaji wa siri za Serikali na muundo wa maendeleo tumishi wa kada ya waandishi na waendesha ofisi, yaliyotolewa na wataalamu waliobobea kwenye fani hizo kutoka serikalini.
“Pia kwenye mkutano huu tumekuwa na kliniki maalumu ya kiutumishi, kazi kubwa ya kliniki hii ilikuwa ni kusikiliza watumishi wa kada hii na kutatua changamoto zao,”amesema.
Zuhura ametaja changamoto wanazokumbana nazo ni baadhi ya waajiri kutowapangia majukumu ya kazi zinazoendana na taaluma yao, badala yake wanapangiwa kazi tofauti, akitolea mfano kukaa mapokezi.
Pia amesema waajiri wengine wameacha kutekeleza muundo mpya wa maendeleo ya utumishi na wengine kutokuwa na mpango wa mafunzo kwa kada hiyo.