Joto kazini laua 18,970 kila mwaka duniani

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza  jijini Arusha kwenye kilele cha maadhimisho ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi, yaliyofanyika leo Jumapili, Aprili 28, 2024 katika viwanja vya General Tyre.

Muktasari:

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema athari za mabadiliko ya tabianchi ni kipengele kimoja cha usalama mahala pa kazi,  kwani mabadiliko hayo yameleta madhara kama mvua zinapopitiliza au ukame wa kupitiliza.

Arusha. Wafanyakazi zaidi ya milioni 22 duniani wanapata madhara ya ajali sehemu za kazi, huku wengine 18,970 wakifariki duniani kote kila mwaka kutokana na ongezeko la joto mahali pa kazi.

Mbali na waajiri kuweka mazingira rafiki sehemu ya kazi, waajiriwa wametakiwa kutambua kwamba wana wajibu wa kuhakikisha wanasimamia usalama wao pindi wawapo kazini.

Hayo yamebainishwa leo Jumapili Aprili 28, 2024 jijini Arusha na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kwenye kilele cha maadhimisho ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi.

Maadhimisho hayo ya kimataifa yameongozwa na kaulimbiu isemayo: “Athari za mabadiliko ya tabianchi katika usalama na afya kazini, sajili eneo la kazi Osha katika harakati za kupunguza athari hizo.”

Biteko amesema wanapoadhimisha siku hiyo,  wadau wanapaswa kukumbuka kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi,  ni kipengele kimoja cha usalama mahala pa kazi kwani mabadiliko hayo yameleta madhara, mvua zinazopitiliza au ukame wa kupitiliza, matokeo yake uchumi katika dunia unayumba.

“Watu wengi wamepoteza maisha, tumeambiwa joto peke yake mahali pa kazi limeathiri watu wengi, zaidi ya milioni 22 duniani wanapata madhara ya ajali, 18,970 wanafariki kutokana na madhara ya ongezeko la joto mahala pa kazi,” amesema.

“Maana yake ni kwamba familia nyingi zimeachwa na wajane, yatima na zimeachwa na mtu aliyekuwa anategemewa kwa lishe ya watoto wake, ameenda kazini amerudi akiwa amefariki maana yake ni mzigo mkubwa na tunasababisha hasara kwenye dunia na uchumi wetu, tukumbushane kupanda miti katika maeneo yetu ya kazi,” ameongeza.

Amesema mfanyakazi akiwa salama kazini, uzalishaji utaongezeka na gharama za uendeshaji kupungua na kuwa ni wajibu mkubwa wa mwajiri kwamba kila rasilimali inayokuja kwako uitunze ili iweze kuwafaa baadaye na kuwa kifo cha mtu mmoja kilichotokea mahala pa kazi hakiwezi kupimwa kwa tarakimu.

“Kifo cha mtu mmoja hasa kilichotokea mahala pa kazi, huwezi kupima kwa tarakimu kwa sababu kwa kufanya hivyo ni kukidogoesha, maoni yangu kifo cha mtu mmoja ni kikubwa na kinahitajika kisitokee mahala pa kazi, nitoe wito kwa waajiri wote kuhakikisha hakuna vifo vinavyosababishwa na mazingira ya kazi,” amesema.

“Na waajiriwa ni watu wa kwanza kulinda usalama wake mahala pa kazi, ukiona kuna mtambo unataka kuuendesha una kasoro na wewe umelazimishwa na mwajiri kuendesha, uwe wa kwanza kusema mtambo huu hauko salama na usihesabike umegoma kwa sababu wewe pia una wajibu wa kulinda usalama wako. Kila mtu athamini maisha yake, anavyokuja kazini anapaswa kurudi nyumbani akiwa salama,” amefafanua.

Dk Biteko ameziagiza taasisi zinazohusika na masuala ya usalama kazini na nyinginezo ikiwemo Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (Osha), Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuondoa vitisho na badala yake kujenga uhusiano mwema na wadau wanaofanya nao kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Osha, Hadija Mwenda amesema wafanyakazi ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya Taifa, lakini maendeleo hayo yanachangiwa na usalama mahali pa kazi.

“Siku hii ina lengo la kukumbushana na kuelimishana kuhusu uwepo wa mazingira salama mahali pa kazi ili kulinda usalama wa nguvu kazi, uwekezaji ambao upo na hatimaye kukuza pato la Taifa, tunahakikisha tunaweka mikakati kuhamasisha majanga yasitokee mahali pa kazi na tutaendelea kusimamia majukumu yetu ili wawekezaji usalama mahali pa kazi na tutaendelea kutoa elimu,” amesema.