Bomu la Dege Eco Village sasa latafutiwa mwekezaji

Muktasari:
Uvumilivu wa fukuto lililodumu kwa miaka mingi ndani ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhusu utekelezaji wa mradi wa Dege Eco Village wenye thamani ya dola za Marekani 653 milioni (zaidi ya Sh1.3 trilioni) umefika kikomo na sasa anatafutwa mwekezaji mwingine atakayeuendeleza mradi huo ambao Rais Dk John Magufuli aliwahi kuuita ni bomu.
Dar es Salaam. Uvumilivu wa fukuto lililodumu kwa miaka mingi ndani ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhusu utekelezaji wa mradi wa Dege Eco Village wenye thamani ya dola za Marekani 653 milioni (zaidi ya Sh1.3 trilioni) umefika kikomo na sasa anatafutwa mwekezaji mwingine atakayeuendeleza mradi huo ambao Rais Dk John Magufuli aliwahi kuuita ni bomu.
Malalamiko ya mradi huo yalianza kutolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye ripoti yake ya mwaka 2013/14, siku chache baada ya kuanza kutekelezwa.
Ingawa utekelezaji wake ulianza akiwa Waziri wa Ujenzi, Juni 25 mwaka 2019, Dk Magufuli alieleza kusikitishwa na mradi huo.
“Mradi huu ni bomu, ni mradi wa hovyo, wa kifisadi, tumeshawaeleza NSSF pamoja na bodi washughulikie, watoe mawazo yao na nyie wananchi mtoe mawazo yenu tuone jinsi gani haya majengo tunaweza kuyatumia,” alisema Dk Magufuli.
Dege Eco Village ni mradi uliodhamiriwa kujenga mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ukianza kutekelezwa Septemba 2014, lakini ukasimama Januari 2016 kutokana na madai ya kuwamo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh179 bilioni, hivyo kutokamilika kwa nyumba za kifahari, hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa iliyotarajiwa kuwepo.
Baada ya takriban miaka saba tangu ujenzi usimame, juzi Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alitangaza zabuni ya kumtafuta mwekezaji atakayeuendeleza mradi huo.
“NSSF inakusudia kuuza mradi mzima wa Dege Eco Village, shirika halitawajibika tena baada ya mauzo haya. NSSF inakaribisha zabuni zilizofungwa kuununua mradi huu kwa viwango vya kimataifa vilivyoainishwa kwenye Kanuni za Ununuzi wa Umma zilizochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 446,” inasomeka sehemu ya taarifa ya NSSF.
Kwa wawekezaji watakaovutiwa kuuendeleza mradi huo, NSSF imesema wanaweza kuutembelea huko Rasi ya Dege iliyopo Kigamboni jijini hapa ili kuukagua na kujiridhisha na mandhari yake kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka saa 7:00 mchana wa Novemba 3, mwaka huu.
Zabuni zote, shirika hilo limesema zinapaswa kuwasilishwa mpaka Novemba 14, saa 9:00 alasiri kabla hazijafunguliwa mbele ya waombaji wote watakaokuwa wamejitokeza kwenye ukumbi wake uliopo ghorofa ya saba katika Jengo la Benjamin William Mkapa.
Utekelezaji ulivyokuwa
Wakati unaanza, mradi huo ulikuwa unaosimamiwa na kampuni ya Hifadhi Builders Limited, iliyoanzishwa na Bodi ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (Ahel), huku ukijengwa na kampuni ya Mutluhan Construction Industry kutoka Uturuki.
Kwenye ripoti ya CAG ya mwaka ulioishia Juni 2015, aliuweka mradi huo kuwa miongoni mwa miradi iliyofisidi fedha za umma baada ya kuingia mikataba bila kufuata utaratibu, kanuni wala sheria.
Ripoti hiyo ilibainisha kwamba mradi huo unaojengwa katika ekari 300 umebainika kila ekari moja ilinunuliwa kwa zaidi ya Sh800 milioni. Kumbukumbu zinaonyesha bodi ya NSSF na Azimio walitiliana saini Novemba 15, 2013 kuendesha miradi.
Katika makubaliano hayo, iliridhiwa kwamba Azimio itatoa ekari 20,000 inazozimiliki eneo la Kigamboni ambazo zinafaa kwa ujenzi wa miji ya kisasa. Ardhi hiyo ilikuwa sawa na asilimia 20 ya thamani ya mradi mzima na ingeongeza fedha kufikisha asilimia 55.
Hata hivyo, Azimio ilitoa ekari 300 zilizoelezwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola 108.9 milioni.
Taarifa hizo ziliwaumiza wazalendo wengi kuliona shirika la umma likinunua ekari moja kwa zaidi ya Sh800 milioni wakati Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mwaka 2012 ilikuwa inauza mita moja ya mraba kwa Sh8,000 hivyo ekari moja kuwa sawa na Sh39 milioni tu.
Kwenye ripoti ya mwaka 2014/15, CAG alisema makubaliano yalionyesha NSSF watakuwa na asilimia 45 ya hisa na AHEL asilimia 55.
Ahel ilitakiwa kutoa ekari 20,000 ambazo ni sawa na asilimia 20 na ingechangia asilimia nyingine 35 zilizosalia kwa kutoa fedha taslimu, huku asilimia 45 ya hisa za NSSF zikiwa ni fedha taslimu pekee, lakini Azimio ilitoa ekari 300.
Wajumbe PAC wanena
Mjumbe wa zamani wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Oliver Semuguruka alisema kwa kuwa uuzaji huo ni uamuzi wa Serikali, litakuwa jambo la busara.
“Kikubwa taratibu za kisheria zifuatwe na faida ipatikane. Kama wameamua kuuza ni jambo jema na bila shaka ni uamuzi wa Serikali,” amesema mjumbe huyo.
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliyekuwa mwenyekiti wa PAC kipindi hicho, amesema “kwa maoni yangu, mradi ule unapaswa kukamilishwa kwa sababu fedha zimeshatumika.”
Zitto amesema ni busara kwa NSSF kutafuta mwekezaji wa kuukamilisha au ichukue uamuzi tofauti iwapo imefanya utafiti wa kina kujiridhisha. “Nashauri mradi ukamilishwe,” amesisitiza.
Wanachama wataka ushirikishwaji
Kutokana na kusuasua kwa baadhi ya miradi inayoanzishwa na mashirika ya hifadhi ya jamii, baadhi ya wanachama wamesema ni wakati mwafaka sasa nao kushirikishwa kwenye vikao vya uamuzi wa matumizi ya uwekezaji unaofanywa na wakurugenzi.
“NSSF inachukua fedha zetu zinazokatwa kwenye mshahara. Menejimenti inajifungia na kuamua iwekeze wapi na izitumie vipi fedha hizi bila kuwa na mwakilishi wa wanachama. Tunahitaji kuwa na uwakilishi katika bodi ya wakurugenzi na tuanze kuwa na mkutano mkuu wa mwaka kujadili mwenendo wa shirika,” amesema Anthony Ndunguru, mwanachama wa NSSF.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga amesema ni suala gumu kwa wanachama kuwa na uwakilishi kwenye bodi za mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Wanachama sio wanaoamua uwekezaji, wao ni wachangiaji tu na uwekezaji unafanyika ili wakihitaji hiyo michango yao waipate. Kama watashirikishwa kwenye bodi, wangapi wataingia? Hii haiwezekani, utaratibu uliopo ni tofauti na kuchangia hisa kwenye kampuni,” amesema.
Amefafanua michango ya wanachama wa NSSF hutolewa si kwa sababu ya kupata faida baadaye, bali ni akiba watakayorejeshewa.
Wasomi wafafanua
Mchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Felician Mutasa amesema ni uamuzi mzuri kwa NSSF kumtafuta mwekezaji mwingine atakayeuendeleza mradi wa Dege Eco Village kuwa hakukuwa na faida ya mradi huo kuendelea kubaki kama ulivyo.
Ameeleza kuwa fedha za ununuzi wa ardhi na kuanza utekelezwaji wake zimetoka kwenye michango ya wanachama na hakuna namna ya kuzirudisha iwapo mradi hautakuwa unaingiza faida, hivyo kuuza ni uamuzi sahihi.
“Wakati wa kubuni nadhani kulikuwa na matarajio ya faida, lakini kilichotokea hatujui undani wake. Kuliko kuendelea kukaa na eneo lililokutia hasara na lisiloingiza faida, kuliuza ni jambo jema,” amesema Dk Mutasa.
Hata hivyo, amesema wakati wa uanzishwaji wa mradi huo kulikuwa na matarajio mengine kulingana na uongozi uliokuwepo ambao, sasa umebadilika na hauoni faida ya kuendelea nao, hivyo ni vema kuuza.
Mchumi Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema mkwamo wa uendelevu wa biashara katika taasisi na mashirika ya Serikali unasababishwa na kukosekana kwa falsafa ya usimamizi wa uchumi.
Falsafa hiyo amesema inataka mshahara wa mfanyakazi utokane na kazi anayoifanya kila siku, akitolea mfano kwenye mradi wowote kwamba ujira wake uzalishwe kutokea hapo, hali ambayo ni tofauti kwa wafanyakazi wa Serikali ambao chanzo cha mishahara yao si kile wanachokifanyia kazi.
“Mtu anayeajiriwa halafu mshahara wake usitokane na sekta anayoisimamia akipewa mradi anakuwa kama mama anavyomlea mtoto yatima au wa kambo. Changamoto za utekelezaji wa falsafa hiyo ndiko kunakozifanya taasisi nyingi za Serikali zinapoanzisha kampuni zishindwe kuzalisha, ukilinganisha na mfanyabiashara binafsi,” amesema.
Tofauti na hali ilivyo serikalini, amesema sekta binafsi itajitahidi kupunguza bei ili izalishe kwa wingi na inasimamia kwa ufanisi kwa sababu inachokisimamia ndicho chanzo cha mshahara wa wafanyakazi waliopo.
Kinachopaswa kufanywa na Serikali, amesema ni kutengeneza sheria zitakazoweka mazingira mazuri na yenye ushindani wa usawa wa kibiashara na ishirikiane na sekta binafsi kwenye miradi yake.
“Sekta binafsi inaposhirikiana na Serikali inafanya kazi vizuri kwa sababu sekta binafsi hujielekeza katika kupunguza gharama ili kupata faida. Mashirika ya umma katika mataifa mengine duniani yameingia ubia na sekta binafsi ili kuendesha miradi kwa faida,” amesisitiza mchumi huyo.
Vilevile, Profesa Aurelia amesisitiza kwamba mkurugenzi wa shirika la umma anapaswa kusimamia sheria katika mchakato wa kuingia ubia na wafanyabiashara binafsi ili kuzalisha kwa tija.