Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi tume haki za binadamu atoa ya moyoni matukio ya utekaji, mauaji

Baadhi ya viongozi wa taasisi zinazohusika na masuala ya maadili na haki za binadamu wakiwa katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dodoma, uliolenga kuzungumzia maadhimisho ya siku ya haki za binadamu itakayofanyika Desemba 10 mwaka huu.

Muktasari:

  • Wakati maadhimisho ya maadili na haki za binadamu nchini yakikaribia, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mathew Maimu ataka matukio ya utekaji na mauaji kufanyiwa kazi kwa kina.

Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Maimu, amesema masuala ya utekaji na mauaji yanayotokea nchini yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa kina, ili kuondokana nayo kwa sababu yanaiharibia nchi.

Jaji Maimu ametoa kauli hiyo kipindi ambacho jamii imeendelea kushuhudiwa mwendelezo wa matukio ya watu kutekwa, kupotea kwenye mazingira tatanishi na wengine kuonekana wakiwa na majeraha.

Matukio hayo yamezidisha hofu miongoni mwa wananchi hususan wanasiasa, wanaharakati na wafanyabiashara. Tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekwisha yakemea na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike na taarifa apelekewe.

Tukio la karibuni ni la Desemba 1, 2024 la Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT- Wazalendo, Abdul Nondo kuchukuliwa na watu wasojulikana.

Nondo alichukuliwa alfajiri katika Kituo cha mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam akitokea Kigoma kwenye shughuli za kisiasa. Jeshi la Polisi likasema linafuatilia kwani alichukuliwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari aina ya Land Cruisers.

Siku hiyohiyo usiku, Nondo alitelekezwa Coco Beach kisha yeye akaomba msaada wa bodaboda wakampeleka makao makuu ya chama chake, Magomeni na sasa anaendelea na matibabu Hospitali ya Aga Khani, Dar es Salaam.

Aidha, tukio jingine ni la Desemba 3, 2024 la Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni, Kata ya Makongorosi Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, Michael Kalinga kukutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa.

Tukio jingie ni lile la kupigwa risasi hadi kufariki dunia kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki Novemba 13, 2024.

Taarifa za awali zinaeleza, tukio hilo lilitokea Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, Wilaya ya Iringa alipokuwa akiishi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga, ambako alifariki dunia.

Wakati matukio hayo yakiendelea na makumi ya watu wakidaiwa kutekwa maeneo mbalimbali nchini huku ndugu, jamaa na marafiki wakiendelea kuwatafuta, leo Alhamisi, Desemba 5, 2024, Jaji Maimu ametoa ya mayoni juu ya matukio hayo ambayo tume yake umewahi kueleza inayafanyia uchunguzi kwenye mikoa 15.

Jaji Maumu amesema hayo jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kuzungumzia kuhusu maadhimisho ya siku ya haki za binadamu ambayo itafanyika  Desemba 10.

Maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu, yatatanguliwa na siku ya mapambano dhidi ya rushwa yatakayofanyika Desemba 9, 2024.

“Naamini hata viongozi wa Serikali hasa akiwemo Rais haridhiki na hali hiyo. Na kama mtakumbuka baada ya tukio lile la kuuawa kwa Ali Kibao  Rais alitoa agizo vyombo vya kiuchunguzi vifanye kazi zake,” amesema.

Amesema hilo linaonyesha Rais Samia Suluhu Hassan hapendezewi na mambo kama hayo yaliyojitokeza kabla na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Changamoto hii inatakiwa kufanyiwa kazi kwa kina ili angalau kuondokana na mambo haya kwa sababu haya yanatuharibia katika maeneo mengi…Jicho la dunia linatuangalia na mara nyingi wanapenda kuangalia mambo ambayo sio mazuri zaidi,” amesema.

Amesema anafikiri ni wakati mwafaka sasa wa kutafakari na kuona wanafanyaje, ili kuondokana na hali hizo ambazo hujitokeza wakati wa uchaguzi.

Kibao ambaye alikuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Septemba 6, 2024 akiwa ndani ya basi eneo la Tegeta Kibo Complex, Dar es Salaam, alitekwa na watu wasiojulikana.

Siku moja baadaye Yaani Septemba 8, 2024, mwili wake uliokotwa ukiwa umetupwa eneo la Ununio huku mwili huo ukiwa umeharibiwa usoni ukidaiwa kumwagiwa tindikali.

Alichokisema Simbachawene

Akizungumza kuhusu siku ya ya haki za binadamu, Waziri Simbachawene amesema maadhimisho ya mwaka huu, yatakuwa ni tofauti kidogo na mwaka jana ambapo wananchi walikutana moja kwa moja na watumishi wa umma ili kupata elimu na huduma.

“Mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika tofauti kidogo ambapo watumishi wa umma watafanya kongamano la tathimini kuhusu uzingatiaji wa haki za binadamu na kuepuka rushwa wanapotoa huduma kwa umma,” amesema.

Amesema watumishi hao watajitathimini ni namna gani wanatekeleza jukumu la Serikali la ustawi wa wananchi, haki za binadamu, kuepuka vitendo vya rushwa na namna wanavyowajibika kwa umma.

Pia amesema taasisi zinazosimamia utawala bora na haki za binadamu zitafanya ziara katika magereza ya Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma, kwa lengo la kuwasikiliza wafungwa na mahabusu na kutoa msaada katika magereza hayo.

Amesema viongozi mbalimbali na watumishi mbalimbali watatoa ufafanuzi wa masuala yanayohusu maadili, haki za binadamu na juhudi za kupambana na rushwa kwenye vyombo vya habari.

Aidha, Simbachawene amesema tathimini ya hali ya maadili ni kuwa watumishi wamekuwa wanafanya kazi nzuri kwenye suala hilo na wale wachache wanaoshindwa kufanya hivyo, wamekuwa wakichukuliwa hatua.

Amesema taasisi zitakazoshiriki kuadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa,  ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ofisi ya Ukaguzi Tanzania (NAOT), Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Tume ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Katiba na Sheria.

Nyingine ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Sektarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti ya Manunuzi ya Umma (PPRA) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).