Bosi Zaeca ajiuzulu

ACP Ahmed Khamis Makarani.

Muktasari:

  • Siku tano baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kuitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) kujitathmini, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, ACP Ahmed Khamis Makarani amejiuzulu.

Dar es Salaam. Siku tano baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kuitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) kujitathmini, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, ACP Ahmed Khamis Makarani amejiuzulu nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Septemba 2, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu-Zanzibar, Charles Hilary, Rais Mwinyi amekubali barua ya kujiuzuluya Makarani.

Taarifa hiyo imesema hatua hiyo inafuata maelekezo ya Rais Mwinyi kuitaka Zaeca kujitathmini, baada ya hivi karibuni kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

Jumamosi ya Agosti 27, 2022, Rais Mwinyi alikabidhiwa ripoti na CAG, Dk Othman Abbas Ali Ikulu Mjini Zanzibar ikianika madudu na ubadhirifu wa fedha za umma.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais Mwinyi aliinyooshea kidole Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca), kuwa haina msaada kwa Serikali.

Rais Mwinyi alisema kama mamlaka zinazohusika zingekuwa zinafanya kazi, isingekuwa kila mwaka yanarudiwa kutajwa mambo yale yale ya ubadhirifu.

“Zaeca lazima mjitathmini sana, hamtusaidii, sijawahi kuona Zaeca wakipeleka kesi mahakamani katika hii miaka miwili ya utawala wa Serikali hii,” alisema Rais Mwinyi

Huku akimpongea CAG, kwa kazi anayoifanya, Rais  Mwinyi alisema iwapo taasisi zenye dhamana ya kushughulikia mambo hayo zingekuwa zinafanya kazi yake wangepiga hatua kubwa.

Akionyesha kusikitishwa kwake, Rais Mwinyi alisema ripoti ya mwaka jana alimpa Zaeca akamuagiza awatafute wenye matatizo, lakini mpaka sasa hajapata majibu yoyote.

 “Kuna wizi mkubwa wa wazi unaotokea Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya na Mamlaka ya Mapato Zanzibar, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa,” alisema

Alisema kuna baadhi ya watu walihusishwa na kukiri kuchukua fedha, lakini hakuna hatua wala kusikia mtu hata mmoja aliyefikishwa mahakamani, “kuna fedha zilizotolewa na Wizara ya Kilimo za ununuzi wa mbolea kinyume kabisa, lakini hatua hazijachukuliwa mpaka leo.”

Hata hivyo, alisema wengi hawapendi kusikia taarifa kama hizo, huku akisisitiza kuwa “lakini CAG endelea kusema ukweli, yapo mengine yana majibu, mengi hayana na huu ndio utakuwa utaratibu wetu wa kila mwaka, lazima tuweke ripoti hizi wazi na huo ndio utawala bora.

Hata hivyo, alisema ukaguzi huo unahusisha Serikali ya awamu ya saba na ya nane. “Maana yake sisi tumeingia zikiwa zimeshapita robo mbili, kwa hiyo yaliyofanyika Serikali hii ilikuwa hawajaingia madarakani. Hivyo sitegemei mambo haya mwaka ujao tuyapate.”