Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Wagonjwa wengi wa shinikizo la damu hawajitunzi'

Muktasari:

  • Haya ni matokeo ya utafiti uliopewa jina "Self Care Practices and Knowledge of Hypertension Management Among Patients Attending Clinics in Tanzania: A Multi Centre Analytical Cross-sectional Study na kuchapishwa katika tovuti ya East African Health Research.

Dar es Salaam. Licha ya idadi kubwa ya wagonjwa wa shinikizo la damu nchini kuwa na uelewa mzuri kuhusu namna ya kudhibiti ugonjwa huo, wengi wao bado hawafuati ipasavyo mbinu za kujitunza zinazoshauriwa na wataalamu wa afya.

Haya ni matokeo ya utafiti uliopewa jina "Self Care Practices and Knowledge of Hypertension Management Among Patients Attending Clinics in Tanzania: A Multi Centre Analytical Cross-sectional Study na kuchapishwa katika tovuti ya East African Health Research.

Utafiti huo ulifanyika katika hospitali zilizopo mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam, ukihusisha wagonjwa 311 wa shinikizo la damu waliokuwa wakihudhuria kliniki.

Lengo kuu lilikuwa kutathmini kiwango cha ufuasi wa mbinu za kujitunza, uelewa wa wagonjwa kuhusu usimamizi wa shinikizo la damu, pamoja na sababu zinazochangia kufuata au kutofuata mbinu hizo.

Matokeo yanaonesha kuwa ni asilimia 25.1 pekee ya washiriki waliokuwa na kiwango kizuri cha kujitunza. Hii ina maana kuwa takribani wagonjwa watatu kati ya wanne hawafuati kikamilifu miongozo muhimu ya kujitunza, hali inayoweza kuongeza hatari ya kupata madhara makubwa ya kiafya kama vile kiharusi, mshtuko wa moyo na matatizo ya figo.

Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa wagonjwa wengi walikuwa na mwenendo mzuri katika baadhi ya maeneo muhimu. Asilimia 76.2 walikuwa wanatumia dawa walizoandikiwa kwa usahihi, asilimia 99 hawakuvuta sigara, na asilimia 95.2 hawakuwa watumiaji wa pombe.

Aidha, asilimia 64.3 walikuwa wakifanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, huku asilimia 59.5 wakifuata mpango wa lishe unaopendekezwa kwa wagonjwa wa shinikizo la damu.

Kwa upande wa maarifa, utafiti umeonesha kuwa asilimia 71.1 ya washiriki walikuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kudhibiti shinikizo la damu. Hata hivyo, watafiti wamebaini kuwepo kwa pengo kubwa kati ya maarifa hayo na utekelezaji wa vitendo vya kila siku vya kujitunza.


Uchambuzi wa takwimu

Uchambuzi wa takwimu umebaini kuwa wagonjwa wenye uelewa mzuri kuhusu usimamizi wa shinikizo la damu walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kufuata mbinu za kujitunza.

Pia, wagonjwa ambao hawakuwa na historia ya ugonjwa huo katika familia zao walionesha ufuasi mzuri zaidi wa mbinu hizo. Kwa upande mwingine, wagonjwa wasiokuwa na magonjwa mengine yanayoambatana na shinikizo la damu walikuwa na uwezekano mdogo wa kuzingatia mbinu za kujitunza.

Watafiti wanasema matokeo haya yanaashiria umuhimu wa kuimarisha elimu ya afya ambayo haitoi maarifa pekee, bali pia inawasaidia wagonjwa kubadili tabia na kuzingatia mbinu za kujitunza katika maisha yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa hitimisho la utafiti huo, juhudi za kudhibiti shinikizo la damu nchini zinapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika kuwajengea wagonjwa ujuzi wa vitendo, huku zikizingatia pia historia ya afya ya familia na uwepo wa magonjwa mengine yanayoweza kuathiri uwezo wao wa kujitunza.

Wataalamu wa afya wanaamini kuwa kuimarisha ufuasi wa mbinu za kujitunza kutachangia kupunguza madhara ya shinikizo la damu, kuboresha ubora wa maisha ya wagonjwa na kupunguza mzigo wa ugonjwa huo kwa mfumo wa huduma za afya nchini.