BoT yapokea maombi manne leseni maduka fedha za kigeni

BOT yapokea maombi manane leseni maduka fedha za kigeni

Muktasari:

  • Serikali imesema hadi kufikia Julai 30 mwaka 2021, Benki Kuu Tanzania imepokea maombi mapya manne ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo yanafanyiwa uchambuzi na wahusika watapewa leseni iwapo watakidhi vigezo.

Dodoma. Serikali imesema hadi kufikia Julai 30 mwaka 2021, Benki Kuu Tanzania (BoT) imepokea maombi mapya manne ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo yanafanyiwa uchambuzi na wahusika watapewa leseni iwapo watakidhi vigezo.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Septemba 10, 2021 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini (CCM) Priscus Tarimo.

 “Nini hatma ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha nchini (Bureau de Change) yaliyofungwa na Serikali nchini kote,” ameuliza Tarimo.

Akijibu swali hilo, Masauni amesema maduka ambayo hayakufungwa yameendelea kufungua matawi na kutoa huduma hizo katika miji mbalimbali nchini.

Amesema kwa ujumla, hali ya upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni nchini Tanzania ni ya kuridhisha.

Aidha Masauni amesema maduka yaliyofungwa pamoja na makampuni mengi yanayotaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini, yanaruhusiwa kuomba leseni Benki Kuu.

Amesema waombaji wanatakiwa kuzingatia matakwa ya sheria za fedha za kigeni ya mwaka 1992 na kanuni za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ya mwaka 2019.

Amesema hadi kufikia Julai 30 mwaka 2021, Benki Kuu ilikua imepokea maombi mapya manne ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo yanafanyiwa uchambuzi na wahusika watapewa leseni iwapo watakuwa wamekidhi vigezo.