Mbunge ataka wafanyabiashara maduka ya kubadilisha fedha kurejeshewa fedha zao

Mbunge ataka wafanyabiashara maduka ya kubadilisha fedha kurejeshewa fedha zao

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania  imetakiwa kufikiri upya kuwarejeshea fedha wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa kuwa baadhi zilichukuliwa bila sababu za msingi.

Dodoma. Serikali ya Tanzania  imetakiwa kufikiri upya kuwarejeshea fedha wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa kuwa baadhi zilichukuliwa bila sababu za msingi.

Hayo yameelezwa na mbunge wa Viti Maalum, Cesilia Pareso wakati akichangia hotuba ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu mwaka wa fedha 2021/22.

Mwaka 2019/20 Serikali ilianzisha msako mkali kwa wafanyabiashara wa maduka ya fedha katika Mkoa wa Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.

Aprili mwaka 2019 aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango katika mkutano wake na waandishi wa habari alibainisha kuwa ukaguzi wa maduka hayo umebaini uondoshwaji wa fedha katika mfumo rasmi na kutekelezwa kwenye utakatishaji wa fedha haramu.

Dk Mpango ambaye sasa ni makamu wa rais wa Tanzania, alisema  katika kazi hiyo iliyofanywa mikoa ya Arusha na Dar es Salaam walibaini pia upokeaji wa amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika.

Katika maelezo yake bungeni leo, Pareso amesema wafanyabiashara walifungua biashara zao kihalali lakini Serikali ilikwenda kuwapora na kusababisha usumbufu mkubwa hata wengine kubaki masikini.

Amesema walikuwa wakifanya biashara zao kihalali lakini hakuna sababu za msingi ambazo Serikali  ilizitumia kuchukua fedha zao.

"Kuna watu wamepoteza maisha yao kwa sababu ya kuchukuliwa fedha zao kwani kuna watu walichukuliwa hadi Sh10 bilioni hivi watu wanaishije namna hiyo," amesema Pareso.

Ametaka viongozi kuisimamia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyosema wafanyabiashara wasisumbuliwe  akitaka iende na vitendo.

Amesema bado wafanyabiashara wanasumbuliwa hadi sasa na akaomba waandikiwe barua ili kuwapa afueni ya maisha.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, wako wafanyabiashara waliopo gerezani kwa kubambikiwa kesi za uhujumu uchumi na makosa mengine na kuomba watazamwe.