Bubelwa aanika sheria inayotaka mkataba wa DP Word kuwa wazi
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitetea usiri wa mkataba kati yake na kampuni ya DP World, Mkurugenzi wa Taasisi ya Fordia, Bubelwa Kaiza, ametaja sheria akisema mkataba huo unapaswa kuwekwa hadharani.
Tangu mkataba wa utekelelezaji (HGA) uliposainiwa Ikulu ya Chamwino mkoaani Dodoma Oktoba 22, Serikali ilisema hayo ni makubaliano ya kibiashara ambayo hayapaswi kuwekwa wazi.
Hata hivyo, akichangia maoni yake leo Jumatano Oktoba 25, 2023 katika mjadala wa Mwananchi Space iliyoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), Kaiza ametaja sheria mbili za rasilimali za mwaka 2017 akisema zinataka taarifa zote za rasilimali za nchi zifikishwe bungeni na kisha kusambaa kwa wananchi.
“Kwa hiyo nadhani haya mambo yakiwa hadharani yakajulikana pengine tunaweza kuwa na uwezo zaidi na kujiamini ya kusema kwamba mkataba huu umekidhi matarajio ya wananchi lakini sio vinginevyo,” amesema Kaiza.
Kwa upande wame mchambuzi wa masuala ya jamii, Faraja Kristomus, amesema ni mapema sana kujua kama mkataba umekidhi matakwa ya Watanzania, kwani hoja yao ilikuwa ni muda wa kuendesha biashara hiyo.
Pia Kristomus amesema, “bado Watanzania wanataka kujua kuwa tutaendelea kusubiri familia nyingine ije kutuendeshea biashara yetu badala ya kuendesha wenyewe kwa manufaa ya kizazi cha sasa kijacho na cha baadaye?
“Watanzania wanataka kujua kuwa ni kweli tumeshindwa kuendesha bandari yetu je sababu ya msingi ni ipi, nafikiri hapa tumekwepa, sababu ya msingi iliyokuwa ikifanya bandari kutokuwa na ufanisi, haijashughulikiwa,” amesema mchambuzi huyo.