Bunge lataka madeni mifuko ya jamii yalipwe

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale akizungumza bungeni alipokuwa akichangia kuhusu taarifa ya shughuli za Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2023, jijini Dodoma leo Februari 7, 2024 . Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka unaoishia Juni 2021, PSSSF ilitoa mikopo ya Sh1.17 trilioni kwa taasisi 10 za Serikali

Dodoma. Bunge limeazimia Serikali iandae mpango unaotekelezeka wa kulipa madeni ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sh1.39 trilioni na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Sh2.45 trilioni.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imesema madeni hayo yanatokana na mikopo ya miradi ya Serikali na michango ya wanachama kwa upande wa PSSSF.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka unaoishia Juni 2021, mfuko huo ulitoa mikopo ya Sh1.17 trilioni kwa taasisi 10 za Serikali zilizokuwa hazijalipwa tangu mwaka 2007.

 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq amesema hayo leo Jumatano Februari 7, 2024, alipowasilisha bungeni taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2023.

Toufiq amesema walibaini changamoto kwenye mfuko wa NSSF ambazo ni kutokamilika kwa mchakato wa kubadili madeni ya Serikali na kuwa hati fungani ya muda maalumu (non-cash bond), hali inayoathiri mapato ya uwekezaji wa mfuko kwa kiasi kikubwa.

Amesema hadi kufikia Juni 2023, deni linalotokana na mikopo iliyotolewa na mfuko kugharimia miradi ya Serikali lilifikia Sh1.39 trilioni, zinazojumuisha Sh624.33 bilioni ambazo ni mkopo halisi na riba ya Sh769.58 bilioni.

Kwa upande wa PSSSF, Toufiq alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uamuzi wa kulipa madeni ya muda mrefu ya Sh2.17 trilioni kupitia hati fungani maalumu, ikiwa ni sehemu ya deni la Sh4.6 trilioni.

Amesema madeni hayo yanajumuisha michango ya wanachama na mikopo ya miradi ambayo mifuko iliyounganishwa iliikopesha Serikali.

“Ni matumaini ya kamati kuwa Serikali italipa deni lililobaki la Sh2.45 trilioni kwa wakati ili mfuko uweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi,” amesema Toufiq.

Amesema, pia kamati imebaini ukiukwaji wa taratibu na kanuni za usajili wa wanachama na uwasilishaji michango kutoka kwa waajiri, hasa iliyo chini ya mshahara halisi wa mtumishi.

Ametaja changamoto nyingine ni waajiri kutotoa mikataba ya ajira na kuandikisha wanachama wachache kuliko waliopo kwenye ajira, hivyo kuathiri uandikishaji wa wanachama na ukusanyaji wa michango stahiki.

Toufiq amesema ipo changamoto ya baadhi ya wastaafu kutopata stahiki zao kwa ukamilifu na kwa wakati, jambo linalosababisha usumbufu kwa wastaafu hao.

Amesema changamoto hiyo imesababishwa na madeni ya malimbikizo ya michango ya wanachama kutolipwa kwa wakati na baadhi ya waajiri, hivyo kuwa na madeni ya muda mrefu ambayo Serikali inadaiwa na mifuko hiyo, jambo linalosababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia Serikali iandae mpango unaotekelezeka wa kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi za jamii ambayo ni mikopo ya miradi ya Serikali na michango ya wanachama kwa upande wa PSSSF,” amesema Toufiq.

Pia, amependekeza NSSF ichukue hatua kali za kisheria kwa waajiri wadanganyifu wanaowasilisha michango iliyo chini ya mshahara halisi wa mtumishi, kutotoa mikataba ya ajira na kuandikisha wanachama wachache kuliko waajiriwa walio nao.


Uchakavu miundombinu UDOM

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Husna Saiboko amesema taarifa za Serikali zimeonesha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kinakabiliwa na uchakavu wa miundombinu, ikiwamo ya maji.

Amezitaja changamoto nyingine ni upungufu wa wahadhiri na uhaba wa mabweni kutokana na baadhi ya majengo yake kutumika kama ofisi za Serikali.

Saiboko  amesema mambo hayo yanakwamisha dhumuni la chuo katika kutoa elimu bora, huku akilitaka Bunge kuazimia Serikali iiwezeshe UDOM kuajiri wahadhiri kulingana na mahitaji.

Pia, amependekeza Serikali iongeze jitihada na kuwa na mkakati wa dhamira wa kutatua changamoto ya maji katika chuo hicho na iongeze kasi ya kukamilisha majengo ya ofisi kwenye mji wa Serikali ili kuacha majengo ya UDOM yatumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa.


Mikopo ya elimu ya juu

Saiboko  amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) inayotegemewa kuweka mifumo na taratibu za kupata idadi kubwa ya wananchi walioelimika, inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo za ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wanaostahili.

Pia, alitaja changamoto nyingine ni kutokupata marejesho ya mikopo kwa walionufaika na wanaoweza kurejesha kutokana na bodi kutoweka mkazo inavyopaswa.

Amesema mambo hayo yanaikwamisha bodi kutekeleza azma yake na kusababisha idadi kubwa ya Watanzania wanaostahili kupata mikopo kutonufaika.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iongeze bajeti ya bodi ya mikopo kwa ajili kuongeza idadi ya wanafunzi elimu ya juu wanaopata mkopo,” amesema.