Mkandarasi apewa mwaka mmoja kulipa michango NSSF

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile wakati akizungumza leo Ijumaa Novemba 10, 2023 bungeni jijini Dodoma.
Muktasari:
- Serikali imembana mkandarasi anayejenga Reli ya Kisasa (SGR), Mwanza - Isaka (Km 341), kuhusiana na michango ya wafanyakazi.
Dodoma. Serikali imemtaka mkandarasi anayejenga Reli ya Kisasa (SGR), Mwanza - Isaka (Km 341) amepewa mwaka mmoja kulipa madeni ya michango ya wafanyakazi katika Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema hayo leo Ijumaa Novemba 10, 2023 alikuwa akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Maswa Magharibi (CCM), Mashimba Ndaki.
Ametaka kujua Serikali inazungumziaje kuhusu malalamiko kuwa mwajiri hapeleki michango ama amepeleka kwa kusuasua
Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema Serikali inatambua kuwa mkandarasi huyo anachangamoto ya kupeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Tayari tumeshaanza vikao kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kukaa naye kuweka ahadi mara tu anapolipwa fedha aweze kupeleka michango hiyo katika mifuko ya hifadhi ya jamii lakini aweze kuwalipa wazabuni mbalimbali,”amesema.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema NSSF imekuwa ikifuatilia kuwa kuna makubaliano wameingia kati ya mfuko huo na mkandarasi ambapo kati ya madeni hayo yanatakiwa kukamilika ndani mwaka mmoja.
“Lakini kuna utaratibu umewekwa kati ya NSSF, kwa wale ambao wanatakiwa kulipa mafao yao sasa utaratibu maalumu wa fedha zao kupatikana ili wasiathirike na malipo hayo. Tutahakikisha tunafuatilia madeni haya ili haki za wafanyakazi zisipotee,” amesema.
Ndaki amehoji mkandarasi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Seke-Malampaka hadi Malya ameajiri wananchi wangapi wanaotoka maeneo hayo.
Akijibu swali la msingi, Kihenzile amesema Serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa SGR kwa kipande cha Mwanza - Isaka (Km 341) kinachojumuisha kipande cha Seke - Malampaka hadi Malya kama sehemu ya mradi huo.
Amesema hadi kufikia mwishoni Agosti, 2023, mkandarasi ameajiri watu 6,793.
Amefafanua kati ya hao, wananchi 1,639 kutoka Mkoa wa Shinyanga, wananchi 1,973 kutoka Mkoa wa Mwanza, wananchi 525 kutoka Mkoa wa Simiyu, wananchi 352 kutoka Mkoa wa Tabora na wanachi 2,304 kutoka mikoa mingine.