Burunge WMA yapewa gari kudhibiti ujangili, migogoro

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo akimkabidhi kadi ya gari Mwenyekiti wa Bodi ya Burunge WMA, Patricia William. Kulia ni Katibu EBN Hunting Safari Ltd, Charles Sylvester

Muktasari:

  • Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA) inaundwa na vijiji 10 na ina ukubwa wa kilomita za mraba 283.

Babati. Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge wilayani Babati Mkoa Manyara, imepewa gari kusaidia kupambana na ujangili na kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu.

Gari hilo aina ya Toyota Land cruiser lenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni, limetolewa na  kampuni ya uwindaji wa kitalii ya EBN Hunting Safari Ltd inayofanya shughuli zake katika kitalu cha uwindaji katika hifadhi hiyo.

Katibu wa EBN Hunting Safari Ltd, Charles Sylvester amekabidhi gari hilo leo Januari 25, 2024 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbongo ambaye naye amewakabidhi viongozi wa Burunge WMA.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Sylvester amesema gari hilo ni sehemu ya makubaliano ya mkataba kati ya EBN na Burunge WMA na baada ya miaka mitano litatolewa gari jingine jipya.

“EBN ina imani gari hili litatumika vizuri ikiwepo kusaidia kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu, lakini pia kukabiliana na ujangili,” amesema.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Anna Mbongo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange, ameipongeza kampuni ya EBN kwa kutekeleza makubaliano ya mkutano kwa wakati.

Amesema gari hilo pamoja na fedha nyingine ambazo zimetolewa na EBN zinapaswa kutumika vizuri kuendeleza uhifadhi na kutatua changamoto za wananchi.

“Vijiji 10 ambavyo vinaunda hifadhi hii ya Burunge vimekuwa na maendeleo makubwa na tuna imani wananchi wataendelea kushiriki katika uhifadhi ili waendelee kunufaika,” amesema.

Meneja mkuu wa Chemchem Association ambayo inashirikiana na EBN, Clever Zulu akisoma salamu za wakurugenzi wa EBN, amesema wana imani katika kuimarika uhifadhi katika eneo hilo.

Zulu amesema EBN Hunting Safari Ltd itaendelea kushirikiana na Burunge WMA na wananchi wa Wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara katika kuendeleza uhifadhi na kuvutia watalii zaidi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Burunge WMA, Patricia William amesema EBN imekuwa na ushirikiano mkubwa katika kuendeleza uhifadhi na Utalii Burunge WMA na wana imani kuendelea kupata ushirikiano mkubwa.

“Gari hili ni sehemu ya makubaliano yetu na watatua gari jingine na tunatarajia pia wataendelea kushirikiana na WMA katika kulinda hifadhi hiyo ili kuendeleza Utalii,” amesema.

Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise ameahidi kutunzwa kwa gari hilo na kuwa litasaidia katika kazi za kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, lakini pia kupambana na ujangili.

Burunge WMA inaundwa na vijiji 10 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 283 ambapo ni hifadhi ya pili ya jamii nchini kwa kuingiza mapato mengi.