Makundi ya wanyamapori yarejea Burunge baada ya kuachwa kuwindwa

Muktasari:

  • Makundi ya wanyamapori ambayo yalikuwa yametoweka katika eneo la Kitalu cha Uwindaji cha EBN, hifadhi ya jamii ya wanyamapori Burunge (Burunge WMA), wilayani Babati, Mkoa Manyara yamerejea na kuanza kuvutia watalii.

Babati. Makundi ya wanyamapori ambayo yalikuwa yametoweka katika eneo la Kitalu cha Uwindaji cha EBN, hifadhi ya jamii ya wanyamapori Burunge (Burunge WMA), wilayani Babati, Mkoa Manyara yamerejea na kuanza kuvutia watalii.

 Wanyamapori aina ya kongoni, pofu, tembo na Simba ambao walikuwa wametoweka katika eneo hilo, sasa wamerejea na kuanza kuvutia maelfu ya watalii.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili Agosti 21, 2022 alisema mwaka huu watalii wamevunja rekodi kutembelea eneo la Burunge WMA na katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

"Hoteli zote za kitalii ndani ya hifadhi na nje zimejaa tunatarajia mapato kuongezeka mwaka 2022/23 na hilo limechangiwa pia na Filamu ya Royal Tour," amesema

Alisema eneo la Burunge WMA na hifadhi ya Taifa ya Tarangire wanaendelea kupokea watalii wengi kwani pia miundombinu imeboreshwa kufika hifadhini.

Naye Mratibu wa kampuni ya EBN, Hunting Safaris, Charles Sylvester anasema ongezeko hilo la wanyamapori limekuwa likivutia watalii kwenda kufanya Utealii wa picha katika Kitalu hicho.

"Tumeweza kurejesha makundi ya wanyamapori wengi ambalo waliopotea hapa kwani licha ya kufanya Utealii wa picha pia tumeboresha mazingira na kudhibiti ujangili" alisema

Kwa upande wake, Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise alisema utalii wa picha umekuwa rafiki kwa wanyamapori lakini pia unawavutia wageni wengi zaidi

"Wanyamapori katika eneo la Kitalu cha EBN wameongezeka na imekuwa rahisi kuonekana ikizingatiwa pia eneo hilo lipo katika mapito ya wanyamapori kutoka hifadhi ya Tarangire kwenda hifadhi ya Manyara," alisema

Alisema mapato ya Utalii katika eneo hilo yameongezeka na vijiji 10 ambavyo vinaunda hifadhi hii mwaka juu vitapata ngao zaidi ya 100 milioni kutoka milioni 19 mwaka 2020/21.