Bwawa la Mindu latapika, kaya 126 zaathirika

Muktasari:

  • Bwawa la Mindu linapokea maji kutoka katika mito mikuu mitano ambayo ni Ngerengere, Lukurunge, Mgea, Mrali na mto Mzinga.

Morogoro. Kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha mkoani hapa, imesababisha Bwawa la Mindu ambalo ndiyo chanzo kikuu cha maji katika Manispaa ya Morogoro na maeneo jirani kufurika na maji kusambaa kwenye makazi ya watu.

Imeelezwa kaya zaidi ya 126 zimeathirika kwa mafuriko hayo.

Akizungumza na Mwananchi jana Alhamis Aprili 4, 2024, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na maji taka Mkoa wa Morogoro, Tamim Katakweba amethibitisha bwawa hilo kujaa na maji kusambaa maeneo mengine.

"Ni kweli bwawa letu la Mindu limejaa kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini na kwa kuwa bwawa letu limetengenezwa kitaalamu zaidi, baada ya maji kufika kwenye vipimo vinavyotakiwa, maji yale yanapitiliza kufuata mkondo na hatimaye humwagika kwenye mto Ngerengere.

Alipotafutwa Joseph Kwitiga, mkuu wa kitengo cha maji juu ya ardhi na usalama wa bwawa kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu, amekiri maji kujaa kwenye bwawa, huku akisema kwa sasa yanamwagika kuelelea Mto Ngerengere.

"Bwawa hili limesanifiwa kuhifadhi maji mita za ujazo milioni 12.6, yakizidi, hupita juu na kumwagikia mto Ngerengere,” amesema.

Amesema hali hii anaifananisha na iliyotokea mwaka jana, ambako mvua zilinyesha juu ya wastani na kusababisha mafuriko maeneo mengi ya Manispaa ya Morogoro.

Kwitika anasema kwa sasa mvua kubwa zilizonyesha kwa mfululizo kati ya Machi 23 mpaka 24, 2024, zimesababisha maji kwenye bwawa hilo kwa takriban lita 73,000 kwa sekunde na kuleta mafuriko katika kidakio cha Mto Ngerengere eneo la Mazimbu.

Hata hivyo, amesema licha ya bwawa hilo kutema, kitu kingine kinachochangia mafuriko ni shughuli za kibinadamu zinazofanyika kando ya mito.

Amesema kazi hizo zimechangia kupunguza kina cha mto sambamba na upana, hali inayosababisha Mto Ngerengere kuhama njia.

Amesema kutokana na madhara yanayotokea mara kwa mara, uongozi wa Bonde umeendelea kutoa elimu kwa wananchi ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya mito, ili kuepusha madhara kama hayo.

Akizungumzia eneo la Mazimbu, ofisa huyo wa Bonde amesema kaya 126 zimekumbwa na mafuriko kutokana na maji hayo.

Amesema asilimia kubwa ya waliokumbwa na mafuriko hayo ni wale waliovamia hifadhi ya mto na kujenga nyumba za kuishi.

“Kumbuka bwawa la Mindu linapokea maji kutoka katika mito mikuu mitano ambayo ni pamoja na Ngerengere, Lukurunge, Mgea, Mrali na mto Mzinga.

"Rai yetu kwa wananchi waliojenga nyumba za makazi kwenye hifadhi za mto Ngerengere wahame, ili waruhusu uoto wa asili uote na kuimarika na kazi kubwa ya uoto ule ni kuzuia ongezeko la tope pamoja na mchanga unaotoka katika milima ambao hupunguza uwezo wa mto Ngerengere kupitisha maji mengi,” amesema Kwitiga.

Wananchi wafunguka

Akizungumza na Mwananchi Digital, mkazi wa Mazimbu, Salvator Hashim amesema mafuriko yaliyotokana na Bwawa la Mindu yamewaathiri kwa kiasi kikubwa.

“Baadhi ya nyumba zimebomoka, maeneo mengi hayapitiki yamezama kwenye maji hatujui tufanyeje sasa, maana hili eneo wakati mwingine hata mvua ikinyesha kidogo tu, yanatokea mafuriko,” amesema Hashim.

Mkazi mwingine,Jamila Shaban ambaye pia ni mkazi wa Mazimbu, amesema baadhi ya maeneo yameathirika kwa kiwango kikubwa na mengine maji hayo yanapita kwa kasi na mengine yametuwama na yameingia hadi kwenye nyumba za watu.

Alipotafutwa Meya wa Manispaa ya Morogoro Paschal Kihanga ambaye pia ni diwani wa Mazimbu, amesema baadhi ya maeneo katika manispaa hiyo hali ni mbaya.

“Hali ya mvua zinazoendelea kama tulivyoambiwa na mamlaka ya hali ya hewa hapa nchini kwamba kutakuwa na mvua za El nino ni kweli tumezipata, lakini kwa sisi hapa Manispaa ya Morogoro zimetuletea madhara makubwa tangu zilipoanza. Nakumbuka mpaka sasa tumeshapoteza watu sita kwa kufa maji,” amesema meya huyo.