CAG ainyooshea kidole Bodi ya Sukari


Muktasari:

  • Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali amebaini kuwa hatua zinazochukuliwa na Bodi ya Sukari (SBT) ikiwamo kuongeza uzalishaji wa ndani wa sukari kwa kuongeza uwekezaji, hazitoshelezi.

Dar es Salaam. Wakati mjadala wa bei ya sukari ukiendelea kurindima na bei ikiwa juu nchini, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) amekosoa juhudi za Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kupambana na uhaba wa sukari, akisema hazitoshelezi.

Kauli hiyo ya CAG imekuja wakati Tanzania ikipita kwenye msukosuko wa uhaba wa sukari uliosababisha bei kupanda, huku Serikali ikieleza kuwa uhaba huo ulisababishwa na mvua za El-Nino.

Alipotafutwa leo kuzungumzia maoni ya CAG, Mkurugenzi Mkuu wa SBT, Kenneth Bengesi amesema hajaiona ripoti hiyo, lakini ataizungumzia atakaporudi nchini akitokea Marekani.

Katika ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma ya mwaka 2022/23, CAG amesema kila mwaka nchi imekuwa ikikabiliwa na hali ya upungufu wa sukari na kuongezeka kwa bei za sukari.

“Hali hii imekuwa ikijirudia bila kuwa na juhudi zinazoenda sambamba na kudhibiti hali hiyo.

“Wakati wa ukaguzi, nilibaini kuwa hatua zinazochukuliwa na Bodi ya Sukari ili kudhibiti upungufu wa sukari nchini hazitoshelezi. Kasi ya hatua zinazochukuliwa ili kuongeza uzalishaji wa sukari wa ndani kwa kuongeza uwekezaji wa ndani ya nchi, bado ni ndogo,” amesema.

Mbali na uzalishaji, CAG pia amesema njia mbadala na za haraka za kudhibiti upungufu wa sukari kwa kuagiza nje kwa wakati, hazitekelezwi kikamilifu.

“Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2022/23 kiwango cha sukari kilichoingizwa kutoka nje ni kidogo, licha ya kuwa kiasi kilichoidhinishwa cha kuagiza sukari kilikuwa kikubwa kwa ajili ya sukari ya majumbani na viwandani,” amesema.

Katika takwimu alizotoa, imeonekana kulikuwa na lengo la kuzalisha tani 490,000 lakini zilizozalishwa ni tani 460,000 kukiwa na upungufu wa tani 29,951.

Pia kulikuwa na vibali vya kuagiza nje 30,000, lakini iliyoagizwa ni tani 6,801 tu na upungufu ulikuwa ni tani 23,199.

Kwa sukari ya viwandani lengo lilikuwa ni kutoa vibali vya kuagiza nje tani 249,880 lakini iliyoagizwa ni tani 196,270, hivyo ukawa na upungufu tani 53,610.

“Nina mashaka juu ya sababu za uwepo wa upungufu huu, hali ya kuwa Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari nyingi zaidi kwa lengo la kudhibiti hali hii.”

CAG amesema kutokuwa na udhibiti wa kutosha wa upatikanaji wa sukari sokoni kunasababisha ongezeko kubwa la bei zisizokotarajiwa, ambazo wananchi wengi hawazimudu.

“Kunasababisha ongezeko la bei za bidhaa za viwandani ambazo zinategemea sukari wakati wa uzalishaji, hivyo kuongeza mzigo wa bei kwa watumiaji wa bidhaa hizo, wengi ambao ni wananchi wa kawaida.


Kilichotokea

Akiuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini kuhusu upungufu wa sukari nchini Februari 22, 2024 Ikulu ya Dar es Salaam, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema kwa miaka miwili iliyopita hakukuwahi kutokea uhaba huo na bei ilikuwa imetulia.

“Kilichotokea ni kwamba mwaka jana tulikuwa upungufu wa tani 30,000 tu, uzalishaji uliongezeka ukafika tani 460,000.

“Miaka yote mvua ipo, uzalishaji unaendelea na huwa tunaagiza kuziba gap (upungufu). Gap yetu imeshguka kutoka tani 200,000 na kidogo hadi kufikia tani 30,000. Mwaka huu tulitaraji kuzalisha tani 550, 000,” alisema Bashe.

Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa ongezeko la mvua na ndio lililosababisha uhaba huo.  

Alisema licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa idhini ya kuagiza tani 100,000, lakini uagizaji utafikia zaidi ya tani 300,000 kwa sababu waliona hali ya mashamba si nzuri.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto ya wafanyabiashara wa rejareja kuongeza bei kiholela na kwamba walikuwa wameshakamata wafanyabiashara 84 wakati operesheni ikiendelea.


Bei elekezi

Januari 23, 2024 SBT ilitoa bei elekezi ya uuzaji wa sukari kwa rejareja isiyozidi Sh3, 200 kwa kilo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, kilo moja ya sukari katika mikoa ya nanda za juu kusini inayojumuisha mikoa Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe ni kati ya Sh2,700 hadi Sh3, 000 na Sh2,600 hadi Sh2,800 kwa jumla.

Kanda ya Mashariki inayounganisha mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani kilo moja itauzwa kwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,000 huku bei ya jumla ikiwa kati ya Sh2,600 na 2,800.

Kanda ya Kati inayobeba na mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora bei ya jumla kwa kilo moja itakuwa Sh2, 650 hadi Sh2, 800 huku bei ya rejareja ikiwa kati ya Sh2, 800 hadi Sh3, 000.

Kanda ya Kusini (Lindi Mtwara na Ruvuma) bei ya jumla itakuwa kati ya Sh2,650 hadi Sh2,900 huku rejareja ikiwa Sh2,900 hadi Sh3,200.

Kanda ya Ziwa inayobebea na mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga Simiyu na Mara bei ya rejareja itakuwa Sh2, 800 hadi Sh3, 000 huku bei ya jumla ikiwa kati ya Sh2,650 hadi Sh2,800.

Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara bei ya jumla itakuwa kati ya Sh2, 600 hadi Sh2,8 00 huku rejareja ikiwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,000.

Kanda ya magharibi inayobebwa na mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa sukari kilo moja bei ya rejareja itauzwa kwa Sh2, 800 hadi Sh3,200 huku bei ya jumla ikiwa kati ya Sh2,600 hadi Sh2,900.