CAG amgusa Sirro mfuko wa maafa Sh4.8 bilioni zilichotwa kinyemela

Aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro katika moja ya tukioakizungumza na waandishi wa habari. Picha na Mtandao

Moshi/Dar. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini Mfuko wa Kufa na Kuzikana wa Jeshi la Polisi nchini ‘uliopigwa’ Sh4.8 bilioni, haukuwahi kufanya vikao vya sekretarieti kwa miaka mitano mfululizo.

Uongozi wa mfuko huo ulikuwa chini ya mwenyekiti na meneja wa mfuko, huku Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) akiwa mwangalizi wa mfuko mwenye jukumu la kuhakikisha miongozo iliyowekwa inafuatwa na kuzingatiwa.

Katika miaka mitano ambayo sekretarieti ya mfuko haikufanya vikao vyake, IGP alikuwa Simon Sirro aliteuliwa kuwa IGP Mei 28, 2017 na kuhudumu hadi Julai 20, 2022 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Taarifa ya ukaguzi maalumu wa CAG, Charles Kichere iliyowasilishwa bungeni Jumatano iliyopita, inasema wamebaini Jeshi la Polisi Tanzania lilikuwa likipokea makato ya fedha kutoka katika mishahara ya askari polisi na wasio polisi (raia) ili kuchangia katika mfuko huo.

Fedha hizi zilikuwa zikiwekwa kwenye akaunti mojawapo ya benki ya kibiashara na zilikuwa zikisimamiwa na makao makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania.

CAG alibaini Jeshi la Polisi lilikuwa likihamisha fedha hizo kwenda akaunti 62 tofauti za benki zilizotengwa kwa ajili ya kulipa mafao ya kufa na kuzikana na zilikuwa katika komandi zote za jeshi zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa CAG, Jeshi la Polisi liliandaa miongozo mahsusi ya kusimamia matumizi ya fedha za mfuko wa kufa na kuzikana na ilihitajika kuanzishwa kwa sekretarieti na uteuzi wa watia saini wa benki.

Wakati IGP alikuwa na jukumu la kuhakikisha miongozo iliyowekwa inafuatwa na kuzingatiwa, meneja wa mfuko alikuwa na jukumu la kupanga vikao vya sekretarieti, huku mwenyekiti alipewa jukumu la kuitisha mikutano mikuu ya mwaka ya wanachama.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi, ilibainika mfuko haukuwa na sekretarieti, hivyo kushindwa kufanya vikao vya sekretarieti kati ya mwaka 2018 na 2022 na haukumwelekeza mwenyekiti wa mfuko kuandaa mikutano mikuu.

“Usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za mfuko huo ulikosekana kwa kuwa hakukuwa na sekretarieti, hivyo kushindwa kufanyika kwa vikao vya sekretarieti na mikutano mikuu ya mwaka ya wanachama,” anasema CAG Kichere

CAG anasema, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), akiwa kama mwangalizi wa mfuko, hakumwelekeza mwenyekiti wa mfuko kuandaa mikutano mikuu ya mwaka ya wanachama.

Jitihada za kumpata Balozi Sirro kuzungumzia suala hili hazikuzaa matunda kwa kuwa simu yake ya kiganjani ilipopigwa kwa ‘WhatsApp’ haikupokelewa, ikiwemo ujumbe mfupi wa maandishi kutumiwa.

Machi 29 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine aliyozungumza kwenye hotuba yake, aliagiza wahusika wote watafutwe kwa hatua zaidi pamoja na kurejeshwa kwa fedha hizo.

Machi 31, mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai akizungumza na gazeti hili kutaka kujua hatua zilizochukuliwa kwa wahusika alisema hatua walishaanza kuzichukua na tayari kesi zimeshafunguliwa mahakamani kwa ajili ya kuwawajibisha askari wote waliohusika na sakata hilo.

“Kwa hiyo tulishachukua hatua kabla ya ripoti ya CAG kuwekwa hadharani na Watanzania waelewe kilichofanyika ni uhalifu kama uhalifu mwingine na wameshughulikiwa kama wahalifu wengine,” alisema.

Kingai katika maelezo yake alifafanua kwa kuweka msisitizo hakuna nafasi yoyote hata akiwa ofisa wa Serikali atakayefanya uhalifu na akafumbiwa macho, watachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwamo kupelekwa mahakamani.

“Kuna mmoja amekimbilia nje ya nchi na tunaendelea kumtafuta kupitia polisi wa kimataifa kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kwa wote waliohusika,” alisema DCI Kingai.


Ubadhirifu wa fedha

Kwa upande wa Tanzania Bara, hadi kufikia Juni 2018, akaunti ya benki ya Mfuko wa Kufa na Kuzikana, iliyokuwa ikisimamiwa na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi katika benki ya biashara, ilikuwa na bakaa ya Sh2.98 bilioni.

Kati ya Julai 2018 na Novemba 2021, mfuko ulikusanya Sh19.27 bilioni na kufanya jumla yote ya fedha za mfuko kuwa Sh22.25 bilioni ambazo zilitolewa katika akaunti ya mfuko na kuhamishiwa kwenye akaunti 62.

Katika kuchunguza matumizi ya fedha zilizotolewa, ilibainika uwepo wa matukio kadhaa ya matumizi mabaya na ubadhirifu unaofikia Sh2.44 bilioni.

Mojawapo ya matukio lilikuwa la watia saini wanne, wakiwamo watatu waliotoroka katika jeshi ili kuepuka kuwajibishwa kwa vitendo vyao, na mmoja aliyestaafu, waliotoa Sh754.65 milioni bila ya kuwapo taarifa zozote za walengwa.

Aidha, ukaguzi ulibaini meneja wa mfuko alijihamishia kwa njia za udanganyifu Sh5 milioni kwenye akaunti yake binafsi ya benki kwa kudanganya kuwa alikuwa miongoni mwa wafiwa.

Hata hivyo, meneja huyo wa mfuko ambaye ripoti ya CAG haikumtaja kwa jina, alikuwa miongoni mwa waliotoroka katika Jeshi la Polisi na hakuweza kupatikana, hivyo kuwa na ugumu wa kumwajibisha kwa vitendo vyake.

Uchunguzi zaidi ulibainisha ushahidi wa meneja wa mfuko kuwashawishi makarani watatu wa Mkoa wa Morogoro na kusababisha kuhamishwa kwa Sh23.50 milioni katika nyakati tofauti kwenda akaunti ya ndugu yake.

Baada ya uchunguzi zaidi ilibainika ofisi ya mkoa wa Kinondoni, askari polisi sita walipokea malipo ya Sh28.20 milioni kwa kisingizio yalikuwa marejesho ya mkopo waliokopesha mfuko na hakuna ushahidi walikopesha.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika, imebainika Mfuko wa Kufa na Kuzikana wa Tanzania Bara ulisimamiwa vibaya na meneja wa mfuko, mwenyekiti na mlezi, walioshindwa kuweka nidhamu na udhibiti katika matumizi sahihi

“Usimamizi huu mbovu ulisababisha ubadhirifu wa Sh2.44 bilioni kutoka kwenye mfuko. Napendekeza hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi ya watu wote waliohusika na ubadhirifu huo, wakiwemo wale waliotoroka,” anasema CAG Kichere.

Uchunguzi huo wa CAG umebaini matukio mbalimbali ya usimamizi mbovu wa fedha za Mfuko wa Kufa na Kuzikana uliofanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar.

Usimamizi huu mbovu ulitokana na kukosekana kwa mifumo mizuri ya usimamizi na udhibiti wa fedha za mfuko uliopaswa kutekelezwa na meneja, mwenyekiti na mlezi wa mfuko.

Kutokana na usimamizi huo mbovu, kumekuwapo na ubadhirifu wa Sh2.40 bilioni uliosababishwa na kuwapo ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi Zanzibar na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania Bara.

“Kulingana na matokeo ya uchunguzi, napendekeza hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi ya watu wote waliohusika katika matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Kufa na Kuzikana.”

CAG anapendekeza Jeshi la Polisi lichukue hatua za haraka za kuanzisha sekretarieti, kuteua mhasibu mwenye uzoefu na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kunakuwepo na utawala bora na usimamizi madhubuti wa fedha za Mfuko.

Wakati CAG akichambua udhaifu wa uendeshaji wa mfuko huo uliosababisha ubadhirifu huo, taarifa zinasema kiutaratibu, mlezi wa mfuko huo alikuwa ni Kamishina wa Utawala na Rasilimali Watu, Kamishna wa Polisi (CP), Benedict Wakulyamba na mikoani walezi ni maofisa wanadhimu au staff officers.

“CP Wakulyamba ndio alikuwa mlezi wa mfuko na ukitizama kesi nyingi zilizofunguliwa polisi kuhusiana na huo wizi mlalamikaji alikuwa Wakulyamba. Halafu naona mnasema waliotoroka ni maofisa wanne tu, sio kweli, hata huko mikoani wako ambao wameingia mitini,” kilidokeza chanzo chetu.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa mmoja wa maofisa wanne waliotoroka aliyetajwa kwa jina la Abdalah alikuwa na nguvu zisizo za kawaida kiasi kwamba alikuwa anaweza kuwaruka maofisa walio juu yake na kuwasiliana moja kwa moja na IGP.

Alipoulizwa aliyekuwa mmoja wa walezi wa mfuko huo, Kamishina Wakulyamba alisema utaratibu ukifuatwa chote kilichozungumzwa kitajibiwa na kwamba yeye siyo msemaji wa jeshi hilo.

“Unajua kuna taratibu za kipolisi ambazo zinatakiwa kufuatwa, ni vizuri ukazingatia hilo na maswali yako yote unayouliza yatajibiwa kwa sababu mimi siyo msemaji wa Jeshi la Polisi,” alisema Wakulyamba.

Alipotafufwa Kamishna wa Utawala na Raslimali watu wa Jeshi la Polisi (SACP), Suzan Kaganda naye alijibu yeye si msemaji wa jeshi hilo na kwamba atafutwe msemaji wa Jeshi la Polisi azungumzie.

Msemaji wa jeshi hilo David Misime alisema: “Ni kweli kulitokea wizi wa Sh4.8 bilioni katika mfuko huo ambazo ni fedha zinazochangwa na askari kwa ajili ya kusaidiana wakati wa msiba. Mfuko huo ni fedha za askari na ni tofauti na taratibu za kisheria zinazofuatwa pale askari au mweza anapofariki.”

Alisema wizi huo ulibainika mwaka 2021 na askari12 walikamatwa na kufikishwa mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali huku akieleza askari wanne walitoroka akiwamo mkaguzi mmoja wa polisi (inspekta) anayesemekana alikimbilia Afrika Kusini.

“Askari hawa bado wanaendelea kutafutwa kwa kutumia mifumo ya ndani na nje ya Tanzania ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani,”alisema Misime.