CAG asema madai ya Sh4.46 bilioni za NHIF yakataliwa

CAG asema madai ya Sh4.46 bilioni za NHIF yakataliwa

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameeleza kuwa Serikali ilipata hasara baada ya kukataliwa madai ya Sh4.48 bilioni za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya  (NHIF)  kutokana na makosa ya ujazaji wa taarifa za wagonjwa.


Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameeleza kuwa Serikali ilipata hasara baada ya kukataliwa madai ya Sh4.48 bilioni za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya  (NHIF)  kutokana na makosa ya ujazaji wa taarifa za wagonjwa.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na idhini batili, kutozingatia miongozo ya matibabu, kutoonyesha vipimo vya utambuzi na kuingizwa kwa huduma ambazo hazikuwa katika mfuko huo.

Hayo yamesemwa leo Aprili 8, 2021 na CAG,  Charles Kichere wakati akiwasilisha ripoti ya mwaka 2019/20 jijini Dodoma akibainisha kuwa madai yaliyokataliwa yanaathiri uwezo wa zahanati, vituo vya afya na hospitali katika kutoa huduma za afya kwa jamii kwani hiyo ni sawa na kutoa huduma za matibabu bure.

“Tathmini niliyofanya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali katika mamlaka 60 za Serikali za mitaa nilibaini uwepo wa madai yaliyokataliwa na mfuko wa Taifa wa bima ya afya ikiwa ni gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaotumia huduma za bima ya kiasi cha Sh2.28 bilioni na Sh2.18 bilioni kwa hospitali za rufaa 26.”

“Hayo yalitokana na makosa katika ujazaji wa taarifa za wagonjwa pamoja na kutozingatia taratibu kama vile idhini batili, kutozingatia miongozo ya matibabu, kutoonyesha vipimo vya utambuzi na kuingizwa kwa huduma ambazo hazikuwa katika mfuko,” amesema Kichere.