CAG: Awajibu wawakilishi waliomtaka aombe radhi

Unguja. Sakata la Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar la kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Dk Othman Abbas Ali kuwaomba radhi limeibuka kivingine, baada ya Dk Ali kuibuka akisema “hao wanajifurahisha.”

Wakati CAG akieleza hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Hesabu za Serikali (PAC), Juma Ali Khatib ameeleza chanzo cha mvutano huo ni wao kumtaka Dk Ali kwenda kubadili kitabu kimoja cha ripoti kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili.

Hayo yanajitokeza siku moja tangu wajumbe hao walipoomba mwongozo wa Spika kuhusu kauli iliyotolewa na CAG, Dk Ali wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2021/22 Mei 3, mwaka huu, Ikulu Zanzibar.

Akiwasilisha ripoti hiyo, CAG alimwomba Rais Hussein Ali Mwinyi kuzijengea uwezo kamati za Kudhibiti Hesabu za Serikali (PAC na LAAC), akisema hazina uwezo katika masuala ya Tehama, akibainisha kuna vitabu vinne ambavyo kamati hizo zimeshindwa kuvifanyia kazi kwa kukosa utaalamu.

Katika kuthibitisha hilo, CAG alisema kamati hizo zimeshindwa kufanya uchunguzi wa mifumo ya Tehama ya Sh1.5 bilioni kwa Wizara ya Afya, Sh1.3 bilioni kwa Wizara ya Ujenzi, Sh5 bilioni katika Wizara ya Fedha ambapo zote zinahusu wizi katika mifumo ya Tehama.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa baraza hilo, ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho, Abdulla Hussein Kombo alisema kiti kitatoa mwongozo baadaye kwa mujibu wa kanuni ya 64 (3) inavyokipa mamlaka hayo. Hadi jana mwongozo haukuwa umetolewa.

Mwananchi ilifika ofisini kwa CAG Ali ili kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya ripoti hiyo, ikiwemo kauli ya wawakilishi waliomtaka awaombe radhi baraza hilo, ambapo licha ya kueleza hataki kuhojiwa na vyombo vya habari, alijibu kwa ufupi akisema ‘wanajifurahisha’, huku akipanda gari lake na kuondoa katika eneo la ofisi yake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa PAC, Juma Ali Khatib alisema kuna kitabu kimoja cha ukaguzi CAG alikiwasilisha kwa Kiingereza kati ya vitabu saba vya ukaguzi.

“Tulimwambia ripoti hiyo aibadilishe, hatuwezi kuifanyia kazi kwa sababu tunatakiwa kujadili Kiswahili na wananchi wapate kufahamu kwa lugha ya Taifa,” alisema na kuongeza:

“Kanuni hasa tunatakiwa tuzungumze Kiswahili na yeye anajua na hoja hii tumeshaitoa barazani, lakini yeye kumbe kaweka kama kiburi, kaja kulisema hapa viwanja vya Ikulu, hiyo ni kubeza, maana tulizungumza tukiwa ndani ya baraza si nje,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema: “Sisi tuna kinga za baraza na hatukumsema vibaya, maana tulinukuu Katiba ya Zanzibar na kanuni za Baraza la Wawakilishi, tukamwambia kwa mujibu wa kanuni zetu tunatakiwa miswada yote inakuja kwa Kiswahili, tunakuomba uilete kwa Kiswahili tulifanyie kazi.”

Khatibu alisema siku zote wakati CAG akiwasilisha ripoti kwa Rais hakuwahi kuwaalika, lakini walishangazwa kuona siku hiyo amewaalika, kumbe ‘anatuita kutuanika na kutunyanyasa mbele ya Rais. Kwa kweli katuchafua na kalichafua Baraza.”

Kuhusu masuala ya Tehama, Khatib alisema, “sisi tumeingia barazani si wahasibu na wala hatujasomea masuala ya fedha, wengine wanasiasa lakini tukiwa pale tunapewa mafunzo kutokana na kamati husika, unaelewa yale mambo ya ukaguzi.”

Alisema kupata mafunzo ni jambo la kawaida, hata kwenye ripoti zao huwa wanasema na kumtaka awapatie mafunzo.
Kutokana na hilo, wamemuomba Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Maulid kuwatafutia wataalamu nje ya ofisi yake ambao watawapatia mafunzo.

Kuhusu kauli ya kwamba wanajifurahisha, alisema CAG anapaswa kujifunza kutumia lugha za staha, kwani wote ni watu wazima na kila mmoja yupo kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.

Hata hivyo, alisema wanasubiri uamuzi wa spika utakaotolewa na kwamba watakubaliana na majibu ya spika kwa kuwa ndivyo kanuni zinavyosema.

Kwa mujibu wa kanuni, majibu ya mwongozo huo yanatakiwa kutolewa kabla ya mkutano wa Bajeti kumalizika Juni 23, mwaka huu.

Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame alisema CAG kajipandisha madaraka makubwa kwamba kamati nzima au baraza hawana uwezo, hivyo alitakiwa kutumia lugha ya kisomi au kistaarabu.

“Huu ni muhimili unajitegemea, kwa hiyo pamoja na madaraka aliyopewa CAG ajifunze kutumia lugha za staha, kuna maneno angeweza kutumia kama vile semina elekezi na yanatumika na wengi wanapewa, lakini kusema hadharani hivyo hakutumia lugha ya kistaarabu,” alisema.

Alisema kuna watu wanapata nafasi kwa sababu za kisiasa na wengine kwa elimu zao, lakini si kwamba anayepata nafasi kwasababu ya kisiasa hana elimu kufanya mambo hayo.

“Kuna wataalamu wengi wanagombea ubunge na hao ndio wanawekwa kwenye kamati, kwa hiyo bila kuchelewa, ni wakati mwafaka wa kuomba radhi kwa sababu si jambo la busara kuelekea kwenye utawala bora.”

Mchambuzi mwingine, Said Hamad Bakar alisema mpaka CAG amefikia hatua ya kutamka hivyo atakuwa ameshaona udhaifu, lakini akaonya kwamba ni vyema wakasuluhisha jambo hilo bila kuleta mpasuko kwa sababu wote wanafanya kazi kwa kutegemeana.

Tukio hilo linafanana na lile la mwaka 2019 ambapo aliyekuwa CAG wa Jamhuri ya Muungano, Profesa Mussa Assad aliingia matatani baada ya kusema Bunge ni dhaifu kwa sababu limekuwa haliisimamii Serikali kutekeleza mapendekezo anayoyatoa kwenye ripoti zake.

Jambo hilo liliibua uhasama kati ya Profesa Assad na Bunge ambapo aliitwa bungeni kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na baadaye kuondolewa kwenye nafasi hiyo kabla ya muda wake wa kustaafu.