Wajumbe Baraza la Wawakilishi wataka CAG awaombe radhi

Mwakilishi wa Mwera Mihayo Juma Suleiman akiomba muongozo kuhusu kauli ya CAG kudai kulidhalilisha baraza hilo kwamba kamati zake hazina uwezo kuchunguza ripoti anazozitoa.

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameomba mwongozo wakitaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuomba radhi chombo hicho kwa kauli yake aliyoitoa mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwamba kamati zake hazina uwezo wa kufanya kazi.

Kauli hiyo wameitoa Mei 5, 2023 wakati wa kikao cha baraza wakiomba mwongozo wa Spika kuhusu kauli iliyotolewa na CAG, Dk Othman Abbas Ali wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2021/22 Mei 3, 2023 Ikulu Zanzibar.

Wakati akiwasilisha ripoti hiyo CAG alimuomba Rais (Dk Hussein Mwinyi) kuzijengea uwezo kamati za Kudhibiti Hesabu za Serikali (PAC na LAAC) akisema hazina uwezo katika masuala ya Tehama maana kuna vitabu vinne mpaka sasa kamati hizo zimeshindwa kuvifanyia kazi kwa kukosa utaalamu.

Katika kuthibitisha hilo CAG alisema kamati hizo zimeshindwa kufanya uchunguzi wa mifumo ya Tehama ya Sh1.5 bilioni kwa Wizara ya Afya, Sh1.3 bilioni Wizara ya Ujenzi, Sh5 bilioni katika Wizara ya Fedha ambapo zote zinahusu wizi katika mifumo ya Tehama.

Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Juma Ali Khatib amesema CAG alitoa kauli zinazoonesha kulibeza na kulidharau baraza hilo tukufu hasa kupitia kamati zake hazina uwezo wa kufanya kazi ripoti zake ikiwemo ripoti ya Tehama.

“Kauli hizo zimekwenda kinyume na kanuni ya 46 ya Baraza la Wawakilishi toleo la mwaka 2020 pia inakwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 sheria ya kinga, uwezo na fursa ya wajumbe wa Baraza hilo namba 6 ya mwaka 2022, Sheria ya Baraza la Wawakilishi namba 6 ya mwaka 2019 ambapo kwa pamoja zinaheshimu haki, fursa na uwezo wa baraza hilo,” amesema.

Amesema baraza hilo linapofanya kazi halipaswi kuingiliwa wnapotekeleza majuku yao.


Aidha walibainisha kuwa CAG anaposema kamati hizo hazina uwezo basi zimemfedhehesha na kumvunjia heshima Spika wa chombo hicho muhimu.    

Juma amabye ni m,wakilishi wa kuteuliwa amesema kauli hizo za CAG zimepokelewa vibaya na jamii ya Zanzibar hasa katika mitandao ya kijamii  zikionesha kuwa Baraza la Wawakilishi na kamati zake hazina uwezo wa kufanya kazi zake hasa katika eneo la usimamzi wa fedha.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Mwanaasha Khamis Juma, aliunga mkono hoja hiyo akisema katiba na kanuni za baraza hilo zinawaongoza.

“Amesema kamati hizi hazina uwezo labda aje atufafanulie uwezo gani ambao alikuwa anautaka kwani kama taaluma na mafunzo moja katika mafungu tunayoyapitisha hapa kuhusu mafunzo kwa kamati za kifedha CAG anapatiwa kwanini asielekeze kuwapatia mafunzo ambayo anahisi sisi wajumbe hatuna uwezo,” alisema

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni ya Baraza la Wawakilishi, Mihayo Juma Nun’ga, amesema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ibara ya 5 imeeleza kuwa taifa litakuwa na mihimili mitatu ikiwemo serikali, mahakama na Baraza la Wawakilishi.


Amesema ibara ya tano kifungu cha tatu imeleeza kuwa hakuna mamlaka itakayoingilia mamlaka nyingine isipokuwa kwa kazi iliyoelezwa katika katiba hiyo.

Mihayo alibainisha kuwa maneno aliyoyasema CAG wakati akiwasilisha ripoti yake kuhusu kamati zake za LAAC na PAAC ni kukikosea heshima chombo hicho cha kutunga sheria.

Amesema CAG amelikosea baraza hilo kwani watu waliokuwepo katika chombo hicho 76 wameaminiwa na wananchi wa Zanzibar hivyo anapotoa kauli mbaya ambazo hazileti taswira nzuri basi anawakosea wananchi wa Zanzibar.

Hata hivyo alishauri kuwa ni vyema chombo hicho kutoa mwongozo kwa kumwita CAG katika kamati yake ya maadili kumhoji na kutoa maelekezo.  

Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho, Abdulla Hussein Kombo amesema kiti kitatoa muongozo baadaye kama kanuni ya 64 kanuni ndogo ya tatu inavyokipa mamlka hayo.