Ripoti ya CAG yatua barazani Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amewasilisha vitabu saba vya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2021/22 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amewasilisha vitabu saba vya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2021/2022 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

Ripoti hiyo inajuimuisha ukaguzi Serikali Kuu, Tawala za Mikoa, Mashirika ya Umma na taasisi zinazojitegemea, na pia mfuko wa maendeleo ya jimbo na wadi, mifumo ya Tehama, miradi ya maendeleo pamoja na ripoti ya kiufundi kwa sekta ya elimu.

Akitoa waraka wa ukaguzi huo, Waziri Haroun amesema jumla ya hati za ukaguzi 160 zimetolewa ambapo kati ya hizo, 146 zinaridhisha, 12 ni zenye shaka, huku moja ikiwa ni mbaya na nyingine ya kushindwa kutoa maoni.

“Kwa upande wa taarifa za hesabu za Serikali kuu jumla ya hati 61 zimetolewa, kati ya hizo, 54 ni zile zinazoridhisha sawa na asilimia 88.5 ya hati zilizotolewa,” amesema

Hati sita ni zenye shaka sawa na asilimia 9.8 ya hati zilizotolewa huku hati moja ambayo imetolewa kwa Wizara ya Maji, Nishati na Madini; ikiwa chafu sawa na asilimia 1.7.

Kwa hesabu za mashirika ya umma na taasisi zinazojitegemea jumla ya hati 41 zilitolewa, kati ya hizo, 35 zinaridhisha ambapo ni sawa na asilimia 85.4 ya hati hote.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa hesabu za Tawala za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, jumla ya hati 44 zilitolewa, kati ya hizo, hati 42 zinaridhisha ambapo hati mbili ni zile zenye shaka.

Kwa upande wa taarifa za hesabu za miradi ya maendeleo jumla ya hati 14 zimetolewa na zote zinaridhisha.

Amesema jumla ya mapendekezo 2,820 yametolewa na CAG kwa mwaka wa fedha uliopita kutoka katika taarifa 182 za ukaguzi wa hesabu zilizoziwasilishwa barazani 2020/21.

“Kati ya mapendekezo hayo, mapendekezo 1,237 sawa na asilimia 43.86 yametekelezwa kikamilifu, huku mengine 659 sawa na asilimia 23.37 yakiwa katika hatua za utekelezaji na 442 ambayo ni sawa na asilimia 15.67; bado hayakutekelezwa,” Amesema.