Kesi anayewashitaki vigogo serikalini yapokelewa

Muktasari:

  • Katika maombi hayo, wanaoshitakiwa ni baadhi ya mawaziri, viongozi wa taasisi za Serikali na mashirika wakituhumiwa kuisababishia Serikali zaidi ya Sh8.4 trilioni.

Dar es Salaam. Thomas Nkola maarufu kwa jina la Mkulima amefungua maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiomba kufungua mashtaka ya kesi tisa ili kuwashtaki baadhi ya mawaziri, wakuu wa taasisi na mashirika wanaodaiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.

Kwa mujibu wa Mkulima, mashitaka hayo yanatokana na ubadhirifu wa fedha za umma uliotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zaidi ya Sh8.4 trilioni.

Wakili anayemwakilisha Mkulima, Penina Ernest alidai mteja wake amefungua kesi hizo chini ya Ibara ya 27 (1) (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo hadi sasa zilizofunguliwa ni tano.

Alidai kuwa mawaziri ambao anataka kuwashtaki ni pamoja na Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa na Mbunge wa Kilosa Profesa Palamagamba Kabudi.

Wengine ni Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkurugenzi wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa.

Wengine ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads), Rogatus Mativila, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutupa, Japhet Justine, Mkurugenzi wa Tanesco Maharage Chande na mfanyabiashara Habinder Sigh Seth.

"Leo ninayo furaha kubwa kuwataarifu umma wa Watanzania kuwa tayari mahakama imepokea na kusajiliwa maombi haya ya kufungua mashtaka ya kesi tisa kwa watuhumiwa kumi," alidai.

Alidai kwenye kesi zote, mteja wake anadai watu hao wamefanya ubadhirifu wa fedha za umma hatua za kisheria zilichukuliwe ikiwezekana warudishe fedha hizo au wafilisiwe.

Ernest alidai kesi hizo ni namba 13, 14, 15,16 na 17 za mwaka 2023 ambazo zimepangwa kwa mahakimu wakuu tofauti wa mahakama hiyo, ambao ni Pamela Mazengo, Huruma Shaidi, Richard Kabate, Evodia Kyaruzi na Mary Mrio.

Pia alidai mteja wake wamewasilidha maombi dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Yapi Merkez, Erdem Arioglu akimtuhumu kula njama na mawaziri wawili na kuiba fedha zaidi ya Sh1.7 tirioni.

Ernest anaeleza kuwa mteja wake anaiomba mahakama hiyo iwachukulie hatua kali za kisheria ikiwemo kuwafilisi mali zao ili kufidia hasara waliyoisababishia Serikali na izuie  mali zao. 

Alidai ktika ripoti ya CAG ya Mwaka 2021/2022 Mwigulu, Tutupa na Japhet wanatuhumiwa kukopa fedha Sh 1.2 tirioni kinyume na bajeti bila ridhaa ya Serikali ambapo inapatikana katika ukurasa 55 na 56 wa ripoti hiyo.

Pia, alidai katika ukurasa wa 32 na 33 wa ripoti ya CAG, washitakiwa Waziri Makamba, Chande na Seth wanatuhumiwa kuisababisa hasara ya Sh342 bilioni.

Katika makosa ambayo mteja wake aliyofungua katika maombi hayo ni kula njama, kuiba fedha za umma, uhujumu uchumi na kusababishia Serikali hasara, matumizi mabaya ya ofisi na kupuuza amri za mahakama.

Wakili huyo alidai maombi hayo ya kesi yanasubiriliwa kupangiwa tarehe za kuanza kusikilizwa.